1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la Taliban lashambulia ikulu Kabul

21 Agosti 2018

Askari wa usalama nchini Afghanistan wamepambana na wanamgambo katika Mji Mkuu wa nchi hiyo Kabul huku helikopta za kijeshi zikifanya mashambulizi juu ya msikiti mmoja.

https://p.dw.com/p/33V54
Afghanistan Raketenangriff auf Kabul
Picha: picture-alliance/AP/R. Gul

Haya ni kwa ajili ya kutuliza msururu wa mashambulizi ya roketi yaliyofanywa na wanamgambo hao. Haikujulikana wakati huo aliyehusika na mashambulizi hayo yaliyotokea wakati ambapo Rais Ashraf Ghani alipokuwa akitoa hotuba ya kuadhimisha siku ya kwanza ya sikukuu ya Kiislamu ya Eid al-Adha, siku chache baada ya kuwapendekezea wanamgambo wa Taliban juu ya usitishaji wa mapigano wa miezi mitatu.

Kulingana na shirika la habari la Associated Press wanamgambo wa Taliban ndio waliofanya mashambulizi hayo ya roketi. Kulingana na afisa wa polisi Jan Agha, roketi ya kwanza ilianguka karibu na ikulu ya rais huku ya pili ikianguka karibu na majengo ya NATO na ubalozi wa Marekani ila hakuna aliyejeruhiwa.

Waliokuwa wakinunua mifugo walionekana wakikimbia

Wanamgambo hao wanadaiwa kujificha katika jengo moja mara baada ya kurusha roketi hizo. Msemaji wa polisi ya Kabul Hashmat Stakankzai amesema karibu washambuliaji 4 na sita wako ndani ya jengo hilo na haijabainika iwapo wameponea mashambulizi ya maafisa hao wa usalama.

Afghanistan Raketenangriff auf Kabul
Maafisa wa usalama wakiwa karibu na eneo la tukioPicha: Reuters/M. Ismail

Watu ambao awali walikuwa wakinunua mifugo kwa ajili ya sherehe ya Iddi walionekana wakikimbia na kujificha huku magari yakipitana kwa kasi na kutoroka mapigano hayo.

"Karibu magaidi wawili au watatu waliingia katika eneo hili na kwa kutumia roketi wakayalenga maeneo kadhaa ya mji wa Kabul. Kwa bahati nzuri hakujakuwa na ripoti za waliofariki, ni polisi wawili tu waliopata majeraha madogo ila wako katika hali nzuri," alisema Najib Danish, msemaji wa wizara ya mambo ya ndani wa Afghanistan.

Eneo hilo ambalo roketi zilirushwa ni mojawapo ya maeneo salama zaidi katika Mji huo Mkuu ambapo majengo ya serikali na ubalozi ambayo yamezungukwa na kuta ndefu yanapatikana. Njia nyingi za kuelekea ubalozi wa Marekani zimefungwa pamoja na njia zinazoelekea majengo ya serikali na jeshi.

Ghani alikuwa ametoa pendekezo la kusitishwa mapigano

Kundi la Taliban  halikutoa taarifa ya moja kwa moja kukiri kuhusika ila shambulizi hilo katika sikukuu hiyo ya Kiislamu linatuma ujumbe mzito. Hili ni pigo pia kwa rais Ashraf Ghani katika juhudi zake za kuwaleta wanamgambo hao katika meza ya mazungumzo ili wavisitishe vita vya miaka 17 vya nchi hiyo.

Afghanistan Raketenangriff auf Kabul
Moshi unafuka kutoka eneo kulikoangushwa roketiPicha: Reuters/M. Ismail

Jumapili iliopita  Ghani alikuwa ametoa pendekezo la kusitishwa mapigano hasa wakati wa sikukuu ya Iddi ila akasema litatekelezwa iwapo kundi la Taliban litakubali. Taliban wamekuwa katika maigano na serikali ya Afghanistan inayoungwa mkono na Marekani kwa karibu miaka 17 na katika miezi ya hivi karibuni, wamezidisha mashambulizi.

Wameteka maeneo ya vijijini na hufanya uvamizi dhidi ya maafisa wa usalama na majengo ya serikali mara kwa mara.

Hapo jana maafisa wa usalama wa Afghanistan waliwaokoa karibu watu 150 wakiwemo wanawake na watoto, masaa machache baada ya wanamgambo wa Taliban kuuvamia msafara wa mabasi na kuuteka nyara katika mkoa wa kaskazini wa Kunduz.

Mwandishi: Jacob Safari/APE/AFPE/DPAE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman