1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirikisho la FIFA lapongeza Kombe la Dunia linavyoendeshwa.

Shisia Wasilwa
29 Juni 2018

Shirikisho linalosimamia kandanda ulimwenguni, FIFA, limepongeza jinsi kombe la dunia linavoyendeshwa nchini Urusi na kutetea mfumo wake wa kuratibu timu zinazoshiriki kwenye makundi. FIFA imesema itaendeleza mfumo huo.

https://p.dw.com/p/30YoC
FIFA Fußball-WM 2018 in Russland | Senegal vs Kolumbien
Picha: Reuters/M. Rossi

Bodi hiyo imeongeza kusema itatumia mfumo huo siku zijazo. Kauli ya bodi hiyo inajiri baada ya timu pekee ya Afrika iliyokuwa imesalia kwenye michuano hiyo ya Senegal kuondolewa na Japan kupitia mfumo huo maarufu wa "Fair Play." 

Mkurugenzi wa Mashindano wa FIFA, Collin Smith, amewaambia waandishi wa habari hivi leo kwamba, utaratibu wa kuangalia kadi za njano na nyekundu zilizotolewa kwa wachezaji wa timu kati ya mwezi Juni 14 na Julai 15 ulitofautisha mchezo wa timu moja na nyingine. Aliongeza kusema kuwa bodi hiyo haikutaka kutumia mtindo wa bahati nasibu kwani timu nzuri inastahili kusonga mbele.

Colins amesema kuwa watatathmini mwenendo wa Kombe la Dunia lakini sio wakati huu, kwani kwa sasa kila kitu ki shwari. Timu ya Senegal ilipoteza nafasi ya kujiunga na timu bora 16 kwani wachezaji wake wawili walikuwa na kadi mbili zaidi za njano dhidi ya Japan kwenye kundi H.

FIFA yapongeza mfumo wa "Fair Play"

Timu zote zilimaliza michuano yao zikuwa na pointi sawa, magoli sawa, kisha timu hizo mbili zikatoka sare zilipokutana, kisha mfumo huo wa "fair play" ukatumika kubainisha timu bora, kinyume na awali ambapo bahati nasibu ilipotumika.

Kocha wa Senegal Aliou Cisse
Kocha wa Senegal Aliou CissePicha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Licha ya kupoteza bao moja kwa nunge kwa Poland, timu ya Japan ilipunguza kasi ya mchezo wake ili kuepuka kadi zaidi, suala ambalo limeibua hisia kali dhidi yao. Walifahamu kuwa Senegal ilikuwa inapoteza mechi yake kwa bao moja kwa sifuri dhidi ya Colombia.

Alipoulizwa kuhusu mbinu ambayo timu ya Japan ilitumia, Smith alisema kuwa anaheshimu utaratibu huo na kwamba ni sehemu ya mchezo.

"Hili ni kombe la kwanza la Dunia ambapo tumetumia kanuni hii iliyotumika awali kwenye michuano ya vijana na kina dada wasiozidi umri wa miaka 20. Lakini ni mara ya kwanza kutumika kwenye kombe la dunia la watu wazima. Tunaamini timu inastahili kusonga mbele kulingana na mchezo wake. Bila shaka tulitaka kuepuka mtindo wa bahati nasibu.” Alisema Smith.

Smith alisema kuwa viwanja vya michuano hiyo vilijaa kwa asilimia 98 katika michuano 48, huku takriban watu milioni 2.2 wakihudhuria. Miji mitano imeandaa kombe hilo ambapo wageni milioni tano wanahudhuria michuano hiyo.

Huku mechi hizo zikiingia awamu ya muondoano wikiendi hii, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi watakuwa vivutio vikuu. 

Timu ya Japan
Timu ya Japan Picha: Reuters/T. Hanai

Drogba: Timu za Afrika zimezembea.

Mabingwa wa mchezo huo, Ufaransa, Argentina, Ureno na Brazil wamewekwa kwenye sehemu moja, huku Uhispania ambayo ni mshindi wa kombe hilo katika miaka ya hivi karibuni ikiwa kwenye sehemu nyingine ya mashindano hayo.

Kati ya timu 16 zilizofuzu kwenye hatua ya muondoano, Argentina inayoongozwa na Messi na ambayo ilikuwa na wakati mgumu kufika kwenye awamu hiyo, sasa itakutana na Ufaransa ambayo inajivunia wachezaji kama vile Antoine Griezmann, Kylian Mbappe na Olivier Giroud, ambao hawajafanya vyema hadi kufikia sasa.

Didier Drogba, aliyeshiriki kombe la dunia na timu ya Ivory Coast, amesema kuwa timu za Afrika zimerudi hatua moja nyuma kwenye michuano hiyo ya Urusi.

     

Mwandishi: Shisia Wasilwa/dpa/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef