1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TBILISI: Rais wa Georgia afutilia mbali madai ya rais Putin wa Urusi

21 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD0P

Rais wa Georgia, Mikhail Saakashvilli, amefutilia mbali uwezekano wa kutumia harakati za kijeshi katika kujaribu kuyarejesha chini ya utawala wa serikali kuu, maeneo mawili ya wapinzani yaliyojitenga nchini humo.

Kiongozi huyo alikuwa akiyajibu matamshi ya rais Vladamir Putin wa Urusi aliyewaambia viongozi wa Umoja wa Ulaya nchini Finnland kwamba Georgia inapania kuyateka kwa nguvu maeneo hayo kwa sababu yanaiunga mkono Urusi.

Viongozi wa maeneo ya Abkhazia na Ossetia Kusini wamethibitisha leo kwamba maeneo yao hayatakubali kurejea katika utawala wa Georgia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirikla habari la Interfax, kiongozi wa Ossetia Kusini, Eduard Kokoity amesema wananchi wa eneo hilo wamechagua uhuru na wanataka kuegemea upande wa Urusi.

Naye rais wa Abkhazia, Sergei Bagapsh, amesema wajumbe wa bunge la mkoa watakwenda Moscow wiki ijayo kuitaka Urusi itambue uhuru wa eneo hilo.