1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tetemeko la ardhi limewauwa zaidi ya watu 1200 Haiti

16 Agosti 2021

Idadi ya waliokufa katika tetemeko kubwa la ardhi nchini Haiti imepanda na kufikia zaidi ya watu 1,200. Waokoaji wanaendelea kuchimba chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka kutafuta manusura.

https://p.dw.com/p/3z2Zv
Haiti | Erdbeben auf Haiti | Zerstörung
Picha: Ralph Tedy/REUTERS

Wakati taifa hilo bado linaandamwa na kiwingu cha mauaji ya rais Jovenel Moise. Huko Les Cayes, kama katika miji mingine iliyoathiriwa sana kusini magharibi, idadi kubwa ya watu walilala nje ya mabaki ya nyumba zao huku kukiwa na hofu ya kutokea matetemeko mapya ya ardhi. Soma zaidi Watu 304 wafa tetemeko la ardhi Haiti

Sauti za vifaa vizito vinavyoondoa mabaki kutoka kwenye majengo yaliyoporomoka zilizagaa mitaani, na ukimya ukitanda miongoni mwa watu wakati wakivuta kwa mkono vifusi katika juhudi za kuwatafuta jamaa zao waliopotea.

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 7.2 katika kipimo cha Richter lililotokea Jumamosi lipiga takriban maili 100 upande wa magharibi mwa mji mkuu wenye wakazi wengi wa Port-au-Prince, ambao pia uliharibiwa vibaya na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea mwaka 2010.

Shirika la ulinzi wa raia limesema majengo 13,600 yameporomoka na zaidi ya 13,700 yameharibiwa, huku mamia ya watu wakifunikwa chini ya vifusi na wengine zaidi ya 5,700 wakijeruhiwa.

Misaada kutoka mataifa mengine

Haiti | Erdbeben auf Haiti | Zerstörung
Waokoaji wakijaribu kufukua vifusiPicha: Joseph Odelyn/AP/dpa/picture alliance

Marekani na mataifa mengine yameahidi kuisaidia Haiti kukabiliana na janga hili la hivi karibuni. Naibu Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Wendy Sherman alizungumza na Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry siku ya Jumapili na kusema kwamba tayari imeweka rasilimali kwa ajili ya kukabiliana na hali ya dharura nchini Haiti. soma Usalama mdogo wakwaza shughuli za uokoaji Haiti.

Mkuu wa shirika la misaada la Marekani, USAID, Samantha Power, kupitia mtandao wa twitter amesema wamepeleka kikosi cha waokoaji 65 kilicho na zana maalum, vifaa na mahitaji ya kimatibabu kujiunga na timu ya kukabiliana na majanga ya tetemeko la ardhi ya Haiti.

Haiti | Erdbeben auf Haiti | Zerstörung
Picha: Joseph Odelyn/AP/dpa/picture alliance

Aidha mataifa kama vile Chile, Argentina, Peru na Venezuela pia yamejitolea kuisaidia Haiti. Umoja wa Mataifa pia umetoa ahadi ya kuisaidia nchi hiyo.

Tetemeko la siku ya Jumamosi lilirejesha kumbukumbu ya madhila yaliyoikumba Haiti Januari mwaka 2010 baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.0 katika kipimo cha Richter kuipiga nchi hiyo ya kisiwa na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 200,000.

 Zaidi ya Wahaiti milioni 1.5 walipoteza makaazi yao wakati wa janga hilo ambalo pia liliharibu asilimia 60 ya mfumo wa sekta ya afya wa Haiti huku viongozi wa kisiwa hicho na jamii ya kimataifa ilikabiliwa na  changamoto kubwa. SomaMustakabali wa Haiti mashakani baada ya mauaji ya rais 

Janga la Jumamosi limetokea wakati nchi hiyo ikikumbwa na mzozo wa kisiasa kufuatiwa kuuawa kwa rais wake, Jovenel Moise mwezi uliopita. Waziri mkuu Ariel Henry ametangaza hali ya dharura ya mwezi mzima na kuwataka Wahaiti kuonyesha mshikamano.

 

Vyanzo:AFP, Reuters