1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May apendekeza kipindi cha mpito baada ya Brexit

22 Septemba 2017

Waziri Mkuu wa Uingereza Thereza May amependekeza kipindi cha mpito cha miaka miwili, ambapo Uingereza itaendelea kuheshimu sheria za bajeti za Umoja wa Ulaya baada ya kuondoka rasmi katika umoja huo.

https://p.dw.com/p/2kY0f
Italien britische Premierministerin Theresa May hält Rede in Florenz
Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May akizungumza mjini ItaliaPicha: picture-alliance/AP Photo/J. J. Mitchell

Uamuzi wa Waziri Mkuu Theresa May kuitoa hotuba yake iliyokuwa ikisubiriwa kwa shauku katika mji wa Florence Italia, umeelezwa kuwa na lengo la kutuma ujumbe wa ''ubunifu na kuanza upya kwa ujenzi wa jamii'', ambavyo vinaambatana na historia ya mji huo wa kale.

Bi Theresa May amerejelea mchakato wa mazungumzo ya Brexit unaoendelea, akisema mchakato huo umekuwa mgumu, lakini akasifu umahiri wa maafisa wakuu wa kila upande katika mazungumzo hayo, David Davis kwa upande wa Uingereza, na Michel Barnier kwa upande wa Umoja wa Ulaya.

Akikumbushia sababu ya waingereza kupiga kura ya kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, May amesema kamwe Uingereza haikuwahi kujisikia nyumbani katika umoja huo, pengine kutokana na sababu za kihistoria na kijiografia. Hata hivyo, amesisitiza kuwa nchi yake itaendelea kutumia raslimali zake katika ushirikiano wa kuhakikisha amani na usalama barani Ulaya.

Haki za raia wa pande zote kuheshimiwa

Florenz, David Davies, Philip Hammond und Außenminister Boris Johnson hören Großbritanniens Premierminister Theresa May zu
Mawaziri David Davis, Philip Hammond na Boris Johnson wakisikiliza hotuba ya Waziri Mkuu Theresa MayPicha: Reuters/J.J.Mitchell

Kuhusu haki za raia wa nchi za Umoja wa Ulaya waishio nchini Uingereza na za Waingereza waishio katika Umoja wa Ulaya, waziri mkuu Theresa May amesema hatimaye haki hizo zitachukua sura mpya, lakini ametoa hakikisho kwa raia wa Ulaya, akianzia na wataliano, kuwa haki zao zitaheshimiwa nchini Uingereza.

Amesema, ''Nataka kurudia, kwamba raia 600,000 wa Italia waishio nchini Uingereza, na raia wote wa Umoja wa Ulaya ambao wamejenga maisha yao nchini mwetu, kwamba tunataka mbakie, na kwamba tunawathamini, na kwamba tunawashukuru kwa mchango wenu kwa maisha yetu kama taifa. Imekuwa na itaendelea kuwa lengo langu kuu katika mazungumzo haya, kuwa mnaweza kuendelea na maisha yenu kama ilivyokuwa kawaida.''

Kipindi cha mpito cha miaka miwili

Italien, Florence, Poteste gegen Theresa May
Kundi dogo la waandamanaji lilikuwepo mjini Florence kumpinga Theresa MayPicha: Reuters/M.Rossi

Katika hatua ambayo inaweza kuwaudhi wakereketwa wa mchakato wa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, Bi May amependekeza kipindi cha mpito cha miaka miwili, ambapo nchi yake itaendelea kuheshimu kanuni za kibajeti za Umoja wa Ulaya, huku ikibakia katika soko la Umoja wa Ulaya.

Theresa May amewapa changamoto viongozi wa Umoja wa Ulaya kuwa wabunifu katika kuweka uhusiano wa baadaye na Uingereza, akisema hapendelei mifumo ya ushirikiano wa kibiashara iliyopo sasa, kama ule uliosainiwa hivi karibuni baina ya Umoja wa Ulaya na Canada. Na amesisitiza historia itawakumbuka kwa ubunifu huo.

''Pale sura ya historia ya Ulaya itakapoandikwa, kitakachokumbukwa sio tofauti baina yetu, bali uwezo wetu wa kutazama mbali, sio changamoto tulizokumbana nazo, bali ubunifu wetu katika kuzitatua, sio uhusiano uliofika kikomo, bali ushirikiano mpya ulioanza. Ushirikiano wa kimaslahi, ushirikiano wa kimaadili, ushirikiano wa nia ya mustakabali wa pamoja''. Amesema Theresa May.

Waziri Mkuu Thereza May amerejelea kauli kuwa kuondoka kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya hakumaanisha kuipa kisogo Ulaya, na kuongeza kuwa itatumia uwezo wake wa kijeshi, kijasusi na kibiashara kwa manufaa ya pamoja ya watu wa Uingereza na nchi za Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, afpe, rtre

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman