1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tillerson ataka mapambanlo dhidi ya IS yaendelee

Josephat Charo
13 Februari 2018

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Rex Tillerson ametoa wito mapambano dhidi ya kundi la dola la kiislamu IS nchini Syria na Iraq yaendelee kuimarishwa.

https://p.dw.com/p/2saNI
Kuwait Außenministertreffen der Koalition gegen die Terrormiliz Islamischer Staat IS
Picha: Getty Images/AFP

Tillerson alisema Marekani itatoa dola milioni 200 kuimarisha usalama katika maeneo yaliyokombolewa nchini Syria, ambayo zamani yalikuwa yakidhibitiwa na waasi.  Akizungumza nchini Kuwait katika mkutano wa muungano unaopambana na kundi la dola la kiislamu, Tillerson pia alisema bado ana wasiwasi kuhusu matukio ya hivi majuzi kaskazini magharibi mwa Syria, na kwamba anaelewa wasiwasi wa Uturuki kuhusu usalama wake.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema leo uamuzi wa Marekani kuendelea kuwafadhili waasi wa kikurdi wa kundi la YPG kutaathiri maamuzi ya Uturuki. Erdogan ameitoa kauli hiyo leo katika hotuba kwa wanachama wa chama chake cha AK bungeni, huku Tillerson akitarajiwa kuzuru nchini humo wiki hii.

Wakati huo huo waasi wa Kikurdi nchini Syria wamesema hawana shida kama serikali ya Syria itawaunga mkono kukabiliana na uvamizi wa Uturuki katika eneo la Afrin. Uturuki imekuwa ikifanya operesheni dhidi ya waasi wa kundi la YPG katika eneo hilo tangu tarehe 20 mwezi uliopita.

Wakimbizi wa Syria wanaofukuzwa Jordan wapungua

Kwa upande mwingine, Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya wakimbizi, Filippo Grandi, alisema idadi ya wakimbizi wa Syria wanaorejeshwa nyumbani kutoka Jordan imepungua kwa kiwango kikubwa katika miezi michache iliyopita, kutokana na miito ya shirika lake kutaka visa vya wakimbizi kulazimishwa kurudi kwao vichunguzwe.

Grandi alisema, "Fikra zangu zinawahusu watu waliokwama katika maeneo yasiyofikika kirahisi nchini Syria, maeneo yaliyozingirwa, huko Ghouta Mashariki, Idlib na kwingineko. Raia lazima waweze kufikiwa na mashirika ya misaada mahala popote walipo."

Schweiz UN-Geberkonferenz Rohingya Flüchtlinge
Filippo Grandi,Kamishan Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na wakimbiziPicha: Reuters/D. Balibouse

Inaaminiwa Jordan imewafukuza maelfu ya wakimbizi kutoka Syria tangu mwaka uliopita, sana sana kutoka na sababu za usalama. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kurejeshwa wakimbizi hao hufanyika haraka, bila uchunguzi wa kina. Grandi aliwaambia waandishi wa habari wakati alipoitembelea kambi ya wakimbizi ya Zaatari nchini Jordan siku ya Jumatatu (12.02.2018) kwamba idadi ndogo tu ya wakimbizi 15,000 wa Syria wameondoka Jordan tangu mwaka 2016.

Grandi aliitolea mwito Marekani na mataifa mengine yaliyostawi kiuchumi kubadili mkondo na kuwapokea na kuwapa makazi wakimbizi zaidi wa Syria ambao wanakabiliwa na hali ngumu. Grandi ataitembelea Syria mwezi ujao kama sehemu ya ziara ya eneo la Mashariki ya Kati iliyoanzia nchini Jordan wiki hii.

Mkutano kuhusu Syria kufanyika Machi

Wakati haya yakiarifiwa, mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Iran na Uturuki wanapanga kukutana mwezi ujao kujadili hali nchini Syria. Hayo yamesemwa leo na waziri wa mashauri ya kigeni wa Kazkhstan, Kairat Abdrakhmanov.

Pande hizo bado zinasubiriwa kutangaza tarehe na mahali mkutano huo utakapofanyika, lakini kuna uwezekano wakakutana mji mkuu wa Kazakhstan, Astana, ambako pia kutaandaliwa awamu mpya ya mazungumzo ya ngazi ya chini kuhusu mzozo wa Syria.

Mwandishi: Josephat Charo/rtre/afpe/dpae

Mhariri: Mohammed Khelef