1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu ya kriketi ya Sri Lanka yashambuliwa Pakistan

K.Küstner - (P.Martin - APE)4 Machi 2009

Nchini Pakistan,watu waliobeba silaha nzito walivamia basi lililokuwa na wachezaji wa timu ya kriketi ya Sri Lanka waliokuwa njiani kwenda kwenye uwanja wa michezo mjini Lahore Wilayani Punjab.

https://p.dw.com/p/H5OC
Bullet holes are seen on a window of a bus, which was carrying the Sri Lankan cricketers, parked outside the Gaffafi stadium after the shooting incident in Lahore, Pakistan on Tuesday, March, 3, 2009. A dozen masked gunmen armed with rifles and rocket launchers attacked the Sri Lankan cricket team as it traveled to a match in Pakistan on Tuesday, wounding several players and killing five police officers, officials said. (AP Photo/K.M. Chaudary)
Alama za risasi katika dirisha la basi lililokuwa likisafirisha wacheza kriketi wa Sri Lanka.Picha: AP

Shambulio hilo limeua polisi 6 waliokuwa wakishindikiza basi hilo.Vile vile wachezaji 7 na msaidizi wa kocha wa timu hiyo walijeruhiwa.Timu ya taifa ya Sri Lanka ilikuwa ikikaribia uwanja wa michezo wa Lahore kushiriki katika mashindano,basi lao liliposhambuliwa na wanamgambo wenye silaha nzito. Kwa mujibu wa Gavana wa Wilaya ya Punjab,mlolongo wa magari yaliyokuwa yakisindikiza wachezaji hao,ulivamiwa na kama wanamgambo 12. Anasema,mtindo uliotumiwa kufanya mashambulio hayo, umekumbusha yale mauaji yaliyofanywa mjini Mumbai nchini India,Novemba mwaka jana.Karibu na eneo la mashambulio ya hiyo jana,si mbali na uwanja wa michezo wa Lahore,vikosi vya usalama vilikuta gruneti na vifaa vya kurushia makombora.

Licha ya mipira ya gari iliyopasuka,dreva wa basi hilo aliweza kuwasalimisha wachezaji hao wa Sri Lanka waliosifiwa kwa kukubali kwenda kucheza nchini Pakistan licha ya kuwepo hali mbaya ya usalama nchini humo.Timu ya India ilikataa kwenda kucheza Pakistan kufuatia mauaji ya Mumbai,Novemba mwaka jana,ikituhumiwa kuwa washambuliaji wametokea Pakistan.Nchini Pakistan,India na Sri Lanka mchezo wa kriketi ni maarufu sana na unapendwa kama vile mpira katika nchi zingine.Waziri wa Michezo wa Pakistan amesema:

"Spoti ni tukio la amani kote duniani.Inasikitisha kuona ukatili usioheshimu hata ujumbe wa amani unaotolewa na wanaspoti na wacheza kriketi."

Timu ya kriketi ya Sri Lanka sasa imesharejea nyumbani,huku zikiwepo shaka iwapo katika kipindi cha hivi karibuni,kutakuwepo timu yo yote ile ya kriketi itakayokwenda kushindana nchini Pakistan na kuhatarisha maisha yao .Wachambuzi wanasema,labda hilo ndilo lengo la magaidi waliofanya shambulio la hiyo jana yaani kuharibu uhusiano wa kirafiki kati ya mataifa;uhusiano unaoimarshiwa kupitia mchezo wa kriketi.Timu za kriketi za India na Pakistan,baada ya kuwa na mvutano wa miaka kadhaa, zilikutana tena uwanjani kwa mara ya kwanza hapo mwaka 2004 .Wakati huo,diplomasia ya kriketi ilifurahiwa kwa shangwe kubwa.Sasa,jirani India imevunjika moyo ikihofia kuwa Pakistan bado haijafanikiwa kudhibiti ugaidi.