1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aagiza ukuta ujengwe kati ya Marekani na Mexico

Caro Robi
26 Januari 2017

Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini amri ya rais kuidhinisha kuanza kujengwa ukuta katika mpaka kati ya Marekani na Mexico. Amri hiyo inalenga kutimiza mojawapo ya ahadi kuu za Trump alizozitoa wakati wa kampeini.

https://p.dw.com/p/2WPkM
Grenze Mexiko - USA
Picha: Reuters/J. L. Gonzalez

Akizuru wizara ya mambo ya ndani hapo jana kutia saini maagizo mawili ya Rais, Trump amewaagiza maafisa nchini Marekani kuanza kazi ya kupanga na kuujenga ukuta huo mpakani akisema nchi isiyokuwa na mipaka sio nchi.

Tayari sehemu ya mpaka huo kati ya Marekani na Mexico ulikuwa umewekewa uzio lakini Trump amesema ukuta unahitajika kuwazuia wahamiaji haramu kutoka nchi hiyo ya Amerika ya kusini kuingia Marekani na pia kuagiza ukaguzi wa mipaka kukamilishwa katika kipindi cha siku 180 zijazo.

Mwaka jana, Trump alisema lengo la ukuta huo ni kuwazuia wahamiaji kutoka Mexico kuingia Marekani kwani huleta matatizo mengi yakiwemo dawa za kulevya, uhalifu na ubakaji. Amesisitiza kuwa gharama ya ukuta huo inayotarajiwa kuwa mabilioni ya dola itagharamiwa na Mexico, suala ambalo serikali ya Mexico imepinga vikali. Bunge la Marekani litahitaji kuidhinisha hatua hiyo ya Rais ili ianze kutekelezwa.

Mexico yaghadhabishwa na hatua ya Trump

Rais wa Mexico Enrique Penna Nieto ambaye anatarajiwa kukutana na Trump wiki ijayo katika ikulu ya White House amelaani agizo hilo la kuanza mara moja kujengwa kwa ukuta mpakani akisema Mexico haiamini kuhusu kuta,wala hawatagharamia ukuta huo bali wanaheshimu nchi nyingine na wanataka pia kuheshimiwa kama taifa huru.

Mexiko Präsident Enrique Pena Nieto gibt neues Kabinett bekannt
Rais wa Mexico Enrique Pena NietoPicha: Reuters/E. Garrido

Uchunguzi wa maoni uliotolewa jana Marekani unaonyesha asilimia 47 ya wapiga kura wanaunga mkono kujengwa kwa ukuta huo dhidi ya asilimia 45 ya wanaopinga. Wataalamu hata hivyo wanatilia shaka iwapo ukuta utazuia uhamiaji haramu au kama unastahili ikizingatiwa mabilioni ya fedha zitakazotumika kuujenga.

Inaripotiwa kuwa kiongozi huyo mpya wa Marekani huenda akasitisha mpango wa Marekani wa kuwapokea wakimbizi kwa miezi minne na kusitisha kutolewa kwa visa kwa wasafiri kutoka kwa nchi saba za Kiislamu, hatua ambayo inatarajiwa kufikiwa leo.

Wakimbizi kuathirika na agizo la Rais

Mpango huo wa wakimbizi utasitishwa kwa siku 120 ili maaafisa wa ngazi ya juu wawasilishe orodha ya nchi zinazoonekana kutokuwa hatari. Maombi yote ya visa kutoka Iraq, Syria, Iran, Sudan, Libya, Somalia na Yemen yatasitishwa kwa siku 30 zijazo.

USA Donald Trump unterzeichnet das Mexico City Dekret
Rais wa Marekani Donald Trump akishikilia agizo la ujenzi wa ukutaPicha: Reuters/K. Lamarque

Pia wizara ya ulinzi itaagizwa kuchukua siku tisini kuwasilisha mpango wa kuundwa kwa maeneo salama Syria au karibu na nchi hiyo ambako wakimbizi wanaweza kupewa hifadhi salama. Kulingana na rasimu ya amri ya rais iliyochapishwa katika vyomvo vya habari vya Marekani ikiwemo Washington post, wakimbizi kutoka Syria watapigwa marufuku kuingia Marekani. Takriban Wasyria 18,000 wako nchini Marekani.

Hatma ya wahamiaji haramu milioni 11 iko mashakani. Huku Trump akionekana kuanza kutekeleza ahadi alizozitoa wakati kwa kampeini kwa kasi, amesema wahamiaji haramu walioingia nchini humo wakiwa watoto hawapaswi kuwa na wasiwasi kuwa watarejeshwa makwao.

Suala jingine ni kuwa anatarajiwa kuagiza tathmini mpya itakayopelekea kurejeshwa kwa mpango wa shirika la ujasusi la Marekani CIA kuwazuia washukiwa wa ugaidi katika maeneo ya siri nje ya nchi ambako mbinu za kuwahoji ni pamoja na matumizi ya mateso.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters/ap

Mhariri: Gakuba Daniel