1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump afuta mazungumzo na kundi la Taliban

Yusra Buwayhid
8 Septemba 2019

Trump amesitisha mazungumzo ya amani baada ya kundi la wanamgambo la Taliban kudai kuhusika na shambulio la mjini Kabul ambalo lilisababisha vifo vya watu 12, akiwemo mwanajeshi wa Marekani.

https://p.dw.com/p/3PE96
Donald Trump
Picha: Getty Images

Rais wa Marekani Donald Trump amesema amevunja mazungumzo ya amani ya kundi la wanamgambo la Afghanistan la Taliban Jumamosi usiku. Katika msururu wa ujumbe aliouandika katika ukurasa wake wa Twitter, amesema alikuwa amepanga kukutana na rais wa Afghanistan pamoja na viongozi wa Taliban nchini Marekani Jumapili.

Trump ameandika Twitter kwamba alivunja mazungumzo hayo baada ya Taliban kudai kuhusika na shambulio la mjini Kabul lilosababisha vifo vya watu 12, akiwemo mwanajeshi wa Marekani.

"Ni watu wa aina gani ambao wako tayari kuua watu wengi ili waonyeshe msimamo imara katika majadiliano?" ameandika Trump katika ukurasa wa Twitter.

"Kama hawawezi kukubali kusitisha mapigano katika mazungumzo haya muhimu ya amani, na wanaweza hata kuwauwa watu wasio na hatia 12, hawawezi kuwa na nguvu ya kujadili makubaliano ya kueleweka," ameongeza Trump.

Mkutano huo ungefanyika, basi ingekuwa ni siku chache kabla ya kutimiza miaka 18 tangu Septemba 11, 2001, yalipotokea mashambulizi ya kigaidi yaliyosababisha vifo 3,000 nchini Marekani. Kundi la Taliban liliwahifadhi wanamgambo wa kundi la al-Qaeda kabla na baada ya kufanya mashambulizi hayo ya kigaidi dhidi ya Marekani.

Afghanistan Selbstmordanschlag in Kabul
Uharibifu wa magari baada ya shmabulio la bomu la kujitoa muhanga mjini Kabul, Afghanistan Septemba 5, 2019.Picha: Reuters/O. Sobhani

Soma zaidi:Watu kadhaa wauawa katika shambulio la bomu harusini

Duru ya tisa ya mazungumzo iliyomalizika hivi karibuni kati ya Taliban na Marekani mjini Doha, Qatar, ilitoa matumaini ya kufikiwa makubaliano kati ya pande hizo mbili kumaliza vita vya miaka 18 nchini Afghanistan.

Ziara iliyopangwa ya Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani kwenda mjini Washington, Marekani ingeweza kuwa hatua moja ya mbele katika kufikia makubaliano hayo.

Kuongezeka kwa mashambulizi hakusaidii juhudi za amani

Makubaliano na Taliban yangehakikisha kuondoka kwa salama kwa maelfu ya wanajeshi wa Marekani katika miezi ya hivi karibuni, katika taifa hilo liloharibiwa kwa vita. Na wanamgambo wa Taliban kwa upande wao wangehakikisha kwamba maeneo yaliyo chini ya udhibiti wao hayatumiki dhidi ya Marekani na washirika wake.

Shambulizi la Taliban lauwa watu 14 Kabul

Kundi la Taliban limeongeza kasi ya mashambulizi Afghanistan hivi karibuni, kuonyesha nguvu yao kwenye uwanja wa vita. Kamanda mwandamizi wa jeshi la Marekani amesema Jumamosi kuongezeka kwa mashambulizi hakusaidii juhudi za amani nchini humo.

Soma zaidi:Shambulizi la kundi la Taliban lawajeruhi watu 95, Kabul

"Haisaidii kitu kwa wakati huu katika historia ya Afghanistan kwa kundi la Taliban kuongeza kasi ya mashambulizi," Jenerali wa majini Kenneth McKenzie, mkuu wa Jeshi kuu la Marekani, aliwaambia waandishi habari waliokuwa wakisafiri pamoja naye.

Wapiganaji wa Taliban walizindua mashambulio katika miji miwili kaskazini mwa Afghanistan, Kunduz na Pul-e Khumri wiki iliyopita na pia mashambulizi mawili ya mabomu ya kujitoa muhanga mji mkuu wa Kabul.

Shambulio moja la Kabul limesababisha kifo cha mwanajeshi wa Marekani kutoka Puerto Rico, Elis A. Barreto Ortiz. Kifo chake kimeifanya idadi kamili ya wanajeshi wa Marekani waliouawa Afghanistan mwaka huu kufikia 16.

McKenzie pia amesema ili mchakato wa amani usonge mbele, "pande zote mbili zijitolee kufikia makubaliano ya kisiasa" ambayo, baadae, yatapelekea kupungua kwa vurugu, ameongeza.

Mapema Jumamosi, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Mark Esper amesema wakati Marekani ikiwa inatafuta makubaliano ya kisiasa na Taliban, haitokubali mpango wowote.

Chanzo: dw