1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump ahusisha mzozo wa Hong Kong na biashara

Admin.WagnerD15 Agosti 2019

Rais Donald Trump ameihimiza China kuutatua mzozo kati yake na waandamanajii wanaotaka demokrasia mjini Hong Kong kwa kutumia njia za kibinadamu.

https://p.dw.com/p/3Nx7O
Handelskonflikt China-USA
Picha: picture-alliance/dpa/S. Walsh

Picha zilizochukuliwa  na shirika la habari la AFP zimeonesha maelfu ya maafisa wa kijeshi wa China wakipeperusha bendera za rangi nyekundu  katika uwanja wa michezo mjini Shenzhen, karibu na mpaka na Hong Kong. Hatua hiyo inajiri huku Rais Trump akihusisha uwezekano wa makubaliano ya kibiashara kati ya nchi yake na China na utatuzi wa amani wa mzozo huo wa kisiasa ambao umeikumba Hong Kong kwa wiki 10 sasa.

Marekani inasema inatiwa wasiwasi na ongezeko la maafisa wa vikosi vya usalama wanaokusanyika karibu na mpaka na Hong Kong, huku kukiwa hakuna dalili ya kusitishwa kwa maandamano hayo kwa upande mmoja na kwa upande mwengine China nayo ikiimarisha ukandamizaji dhidi ya vuguvugu linalotaka mageuzi ya kidemokrasia.

Hongkong | Proteste gegen das Auslieferungsgesetz am Hong Kong international airport
Waandamanji Hong Kong wapiga kambi katika uwanja wa ndege wa eneo hiloPicha: Reuters/T. Siu

Katika ujumbe wake kupitia mtandao wa Twitter, Trump alipendekeza mkutano na Rais Xi Jinping wa China kusaidia kuutatua mzozo huo. Katika ujumbe huo, Trump ameongeza kuwa kama China inataka kuingia katika makubaliano, itabidi kwanza ishirikiane na Hong Kong kwa njia ya kibinadamu na kwamba hana hofu kuwa Rais Xi anataka kutatua mzozo huo mara moja kwa njia za kiutu.

Trump, ambaye amekuwa akitafuta mkataba mkubwa na kurekebisha ukosefu wa usawa wa kibiashara na China kabla ya kampeni yake ya kuwania muhula wa pili wa urais mwakani, amekabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa bunge la nchi hiyo kwa kutochukuwa hatua thabiti kuhusiana na suala la Hong Kong na kutaja maandamano hayo mwanzoni mwa mwezi huu kuwa ghasia ambazo ni suala linalopaswa kushughulikiwa na China.

Wanaharakati bado wanapanga misururu ya maandamano makubwa mwishoni mwa juma hili katika juhudi za kuendeleza azma yao inayoungwa mkono na umma, licha ya ghasia zilizoshuhudiwa wiki hii walipopiga kambi katika uwanja wa ndege wa eneo hilo na kutatiza shughuli za kawaida.

Maandamano ya Hong Kong yalichochewa na mpango uliopingwa wa kuruhusu washukiwa wa makosa mbali mbali kuhamishwa kutoka eneo hilo hadi China Bara na sasa yamegeuka kuwa vuguvugu linalotaka mageuzi ya jumla ya kidemokrasia