1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aiondoa Marekani mkataba wa Tabianchi

Bruce Amani
2 Juni 2017

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuiondoa Marekani kutoka kwenye makubaliano kuhusu mabadiliko ya tabia nchi yaliyoafikiwa mjini Paris, Ufaransa ikiwa ni mojawapo ya ahadi alizotoa wakati wa kampeni.

https://p.dw.com/p/2e0my
USA Trump zum Pariser Klimaabkommen
Picha: Reuters/K. Lamarque

Katika hotuba yake kali aliyotoa kutoka Ikulu ya White House, Rais Donald Trump alisema Marekani itasitisha maramoja utekelezaji wa makubaliano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Huku akitumia kauli mbiu ya "Marekani Kwanza” ujumbe aliotumia wakati alichaguliwa kuwa rais mwaka jana, Trump alisema Mkataba wa Paris utajuhumu uchumi wa Marekani, utawafanya Wamarekani kupoteza kazi, kudhoofisha uhuru wa Marekani na kuiweka nchi hiyo milele katika hali ya kutumiwa na mataifa mengine duniani.

Trump amesema Wamarekani hawataki viongozi wengine na nchi nyingine kuwacheka, na hatoruhusu hilo. Alisema mkataba huo uliosainiwa wakati wa utawala wa mtangulizi wake Barack Obama, unawaweka katika nafasi nzuri wapinzani wa nchi hiyo kiuchumi ambao ni India, China na bara la Ulaya

G7-Gipfel - Trump und Merkel
Anfela Merkel na viongozi wa Ulaya wamekosoa uamuzi wa Trump kuiondoa Marekani katika mkataba wa ParisPicha: Reuters/T. Gentile

Rais huyo wa Marekani hakutoa maelezo  kuhusu ni vipi au lini, mchakato rasmi wa kujiondoa utaanza, na kwa wakati mmoja aliashiria kuwa mazungumzo mapya huenda yakafanyika. Ni wazo lililopigwa maramoja na washirika wa Marekani barani Ulaya waliojawa na hasira, ambao waliungana na viongozi kutoka kote Marekani kulaani hatua ya Trump. Katika taarifa ya pamoja, Ufaransa, Ujerumani na Italia zimesema makubaliano hayo hayawezi kujadiliwa upya.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameiitia hatua hiyo kuwa ya kukatisha tamaa kabisa, na kuwa mkataba huo wa Umoja wa Mataifa hauwezi kujadiliwa upya kwa kuzingatia ombi la taifa moja. Miongoni mwa walioiokosoa hatua ya Trump nchini Marekani ni rais wa zamani Barack Obama ambaye amesema Marekani inajiunga na mataifa machache yanayoukataa mustakabali wa dunia. Nicaragua na Syria ni nchi pekee ambazo hazikusaini makubaliano ya Paris.

Magavana wa Democratic wa majimbo ya New York, California na Washington wameunda muungano wa haraka, wakiapa kuheshimu viwango vilivyokubaliwa chini ya mkataba wa Paris.

Trump aliwapigia simu Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May – pamoja na wa Canada Justin Trudeau – ili kuufafanua uamuzi wake. 

Frankreich Fernsehansprache von Präsident Macron - Pariser Klimaabkommen
Rais Macron amesema Ufaransa haitashirikiana na Marekani kuhusu suala la TabianchiPicha: Getty Images/AFP

China na Marekani huchangia asilimia 40 ya gesi chafu ulimwenguni na watalaamu walionya kuwa ni muhimu kwa nchi hizo mbili kubakia katika makubaliano ya Paris ili yaweze kufanikiwa.

Mjini Berlin, Kansela Angela Merkel alielezea kusikitishwa kwake na hatua hiyo na akatoa wito wa kuendelezwa seza za tabianchi ambazo zitauhifadhi ulimwengu. Mjini Paris, Rais Emmanuel Macron alisema Ufaransa na Marekani zitaendelea kushirikiana lakini sio kuhusu suala la mabadiliko ya Tabianchi. Mjini London, Waziri Mkuu Theresa May alimwambia Trump kuwa mkataba wa Paris unalenga kuvilinda vizazi vijavyo. Jean-Claude Juncker, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya ameishutumu hatua hiyo akisema ni mbaya kabisa.

Ikulu ya White House imesema itaheshimu sheria za Umoja wa Mataifa za kujiondoa kutoka kwa mkataba huo. Sheria hizo zinahitaji taifa kusubiri miaka mitatu kuanzia tarehe ambayo mkataba huo uliidhinishwa kisheria, Novemba 4, 2016 kabla ya kuanza kujiondoa rasmi. Nchi hiyo kisha lazima isubiri mwaka mwingine mmoja. Mwafaka wa Paris unazitaka nchi 195 zilizotia saini kupunguza utoaji gesi inayochafua mazingira ambayo husababisha ongezeko la joto duniani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo