1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aliomba usaidizi wa China katika uchaguzi-Kitabu kipya

Daniel Gakuba
18 Juni 2020

Rais Donald Trump alimuomba rais wa China Xi Jinping kumsaidia kushinda uchaguzi ujao. Hiyo ni mojawapo ya shutuma zilizomo katika kitabu kipya kilichoandikwa na John Bolton aliyekuwa mshauri wake wa masuala ya usalama.

https://p.dw.com/p/3dyXs
USA Präsident Donald Trump und Sicherheitsberater John Bolton
Picha: Getty Images/AFP/B. Smialowski

Katika kitabu chake hicho alichokipa jina la ''The Room Where it Happened'', maana yake, Chumbani Yalipotokea, John Bolton ambaye alikuwa mshauri mkuu wa  Rais Donald Trump kuhusu usalama wa taifa, anasema sera nzima ya rais huyo kuhusu nchi za nje inajikita katika kuhakikisha kwamba anashinda muhula wa pili katika uchaguzi wa Novemba mwaka huu wa 2020.

Dondoo za kitabu hicho tayari zimevuja na kuchapishwa na magazeti kadhaa maarufu ya nchini Marekani, zikimuonyesha Trump kuwa na ujinga wa kiwango cha juu kuhusiana na siasa za kimataifa.

Aiomba China kumpiga jeki ili ashinde uchaguzi wa 2020

Bolton ameandika kwamba katika mkutano mmoja baina ya Rais Trump na mwenzake wa China Xi Jinping, kwa hali ya kushangaza Trump alibadilisha mada ya mazungumzo na kuingiza uchaguzi wa Marekani, akisema China inao uwezo wa kiuchumi ambao unaweza kuleta mabadiliko chanya katika kampeni yake, na kumuomba rais Xi kuhakikisha kwamba Trump anapata ushindi.

Donald Trump, Xi Jinping
Rais Donald Trump wa Marekani (kushoto) na mwenzake wa China, Xi Jinping walipokuwa wakihudhuria mkutano nchini Japan mwaka 2019.Picha: picture alliance/AP Photo/ S. Walsh

Mshauri huyo wa zamani wa masuala ya usalama amesema Trump alizungumzia umuhimu wa wakulima wa Marekani, na jinsi ikiwa China itanunua kwa wingi mazao yao, hilo linaweza kushawishi matokeo ya uchaguzi ujao.

Tuhuma nyingine nzito inayotolewa na Bolton katika kitabu chake dhidi ya Rais Trump ni namna wakati mmoja rais huyo alivyokuwa tayari kufumbia macho ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na serikali ya China dhidi ya watu wa jamii ya Uighur ambao ni Waislamu, akimwambia Rais Xi Jinping kwamba kuwafungia watu hao katika kambi za vizuizi ni hatua sahihi kabisa.

Hesabu za ushindi

Katika dondoo ya kitabu hicho iliyochapishwa na magazeti ya The Washington Post, The New York Times na The Wall Street Journal, Bolton anasema hata akifikiria vipi hawezi kukumbuka uamuzi wowote muhimu wa Rais Trump, ambao haumbatani na hesabu za kushinda muhula wa pili.

Soja Anbau Monokultur
Wakulima wa Marekani ni tegemeo kubwa la Rais Donald Trump kisiasaPicha: Norberto Duarte/AFP/Getty Images

Kama ishara ya namna kitabu hicho kilivyomghadhabisha Rais Trump, wizara ya sheria mjini Washington jana jioni iliwasilisha kesi mahakamani katika hali ya dharura, kutaka uzinduzi wa kitabu hicho cha John Bolton uzuiliwe.

Wizara hiyo imemshutumu mwandishi wa kitabu hicho kutotoa muda wa kutosha ili kitabu hicho kikaguliwe kwanza kama inavyotakikana kisheria, na kutaka mahakama iiingilie kati kukizuia, kuepusha kitisho cha usalama wa taifa kinachoweza kufuatia kutolewa kwake.

Trump mwenyewe amemshambuliwa mshauri wake wa zamani; akizungumza kupitia kituo cha televisheni cha Foxnews amesema John Bolton ni mtu aliyechujuka, ambaye amebobea katika kutoa habari za uongo.

afpe, dpae