1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump asema hatahudhuria kuapishwa kwa Biden

Zainab Aziz
9 Januari 2021

Rais wa Marekani Donald Trump anayeondoka madarakani, amesema hatahudhuria sherehe za kuapishwa kwa rais mpya Joe Biden hapo tarehe 20 ya mwezi huu.

https://p.dw.com/p/3niMi
US-Präsident Donald Trump
Picha: Donald J. Trump via Twitter/REUTERS

Trump amesema hayo wakati ambapo taarifa za vyombo vya habari nchini Marekani zimeashiria uwezekano wa rais huyo kukabiliwa na mashtaka kwa mara ya pili juu ya kumwondoa madarakani baada ya wafuasi wake kulivamia bunge na kufanya fujo.  Uamuzi wa Trump unakingamana na kauli aliyotoa hapo awali juu ya kuhakikisha mchakato wa kukabidhi madaraka kwa amani. Hata hivyo rais mteule Joe Biden amesema uamuzi huo wa Trump ni jambo zuri kwake.

Shirika la habari la Reuters limekinukuu chanzo katika utawala wa Trump kilichotoa taarifa kwamba huenda rais huyo anayemaliza muda wake ataondoka kutoka kwenye Ikulu siku moja kabla ya sherehe za kuapishwa rais mpya wa Marekani na atelekea katika nyumba yake ya mapumziko jijini Florida.

Wabunge wanatarajiwa kujadili hatua za kuwasilisha nakala za mashtaka kwa Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kupiga kura juu ya madai dhidi ya rais Trump ya kuwachochea waandamanaji waliolivamia jengo la bunge la Marekani. Msemaji wa Ikulu, Judd Deere alijibu haraka kwamba kumfungulia mashtaka rais Trump wakati ambapo zimebakia siku 11 tu kabla ya kumalizika kipindi chake cha urais ni hatua itakayoitumbukiza zaidi nchi hiyo katika migawanyiko.

Rais Mteule wa Marekani Joe Biden
Rais Mteule wa Marekani Joe BidenPicha: Kevin Lamarque/REUTERS

Wakati huo huo wabunge wa vyama vyote viwili pamoja na viongozi waandamizi katika utawala wa rais huyo wameanza mazungumzo juu ya kumwondoa madarakani. Spika wa bunge Nancy Pelosi amesema Baraza la Wawakilishi liko tayari kuchukua hatua ikiwa Makamu wa Rais Mike Pence hatakuwa tayari kuitumia sehemu ya 4 kwa mujibu wa kipengele cha 25 cha katiba ya Marekani kinachomruhusu makamu wa rais kuchukua hatua hiyo ikiwa rais ameshindwa kuyatimiza majukumu yake. 

Pelosi amesema wanaweza kupiga kura juu ya kuondolewa Trump ofisini wiki ijayo. Amesema ikiwa Trump hataondolewa kwa njia hiyo bunge litajaribu kwa mara ya pili kumfungulia mashtaka juu ya kumwondoa madarakani.  Spika Pelosi moja kwa moja amemlaumu raisTrump kwa kuchochea alichoita uasi wa kutumia nguvu dhidi ya Marekani.

Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi
Spika wa Bunge la Marekani Nancy PelosiPicha: picture-alliance/newscom/UPI Photo/K. Dietsch

Wakati huo huo idara ya sheria imetangaza kuwa imewafungulia mashtaka watu 15 waliohusika katika vurugu hizo, pamoja na mtu mmoja anayetuhumiwa kuwa na mabomu yakujitengenezea nyumbani. Rais analaumiwa kwa kuwachochea wafuasi wake na amekosolewa kwa kushindwa kulaani vurugu hizo kwa wakati na badala yake alionekana kutetea fujo zilizofanywa na wafuasi wakehao.

Licha ya Trump kusema hatahudhuria sherehe za kuapishwa rais ajae Joe Biden hapo Januari 20, Makamu wa Rais Mike Pence anatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo.

Trump atakuwa rais wa kwanza aliye madarakani kukosa kuhudhuria hafla ya kuapishwa rais mpya wa Marekani tangu wakati wa aliyekuwa rais wa 17 wa Marekani Andrew Johnson. Ni jadi ya Marekani kwa rais anayeingia na yule anayeondoka kuhudhuria sherehe za kuapishwa pamoja ikiwa ni ya kukabidhiana madaraka kwa amani katika taifa hilo kubwa.