1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atangaza sera yake kuhusu usalama

Jane Nyingi16 Agosti 2016

Mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump ameeleza mpango wake wa kuwahakikishia usalama wao Wamarekani.

https://p.dw.com/p/1Jj1r
Picha: Reuters/E.Thayer

Hata hivyo hakueleza bayana jinsi utakavyofanikishwa mpango huo, muda utakaochukua na watakavyogharamika walipa kodi.Trump ambae awali alikuwa amependekeza kupigwa marufuku kwa muda Waislamu kuingia Marekani , ameapa kubadilisha sera za mambo ya nje za nchi hiyo ili kukabiliana na wanaunga mkono makundi yenye itikadi kali na wasiofuata maadili ya Marekani.

Katika hotuba yake juu ya sera za uhamiaji aliyoitoa katika jimbo lenye ushindani mkubwa la Ohio, Trump amesema Marekani inahitaji kushirikiana na mataifa yote ambayo yanataka kukabiliana na ugaidi. Mgombea huyo wa chama cha Republican alisema baadhi ya mapendekezo yake muhimu katika kukabiliana na hali hiyo ni kuliangamiza kabisa kundi la dola la kiislamu IS. Amesema Vyombo vya serikali vitahitajika kuwahoji kwa kina wanaotaka kuingia katika ardhi ya Marekani, kuyafwatilia maisha yao katika mitandao ya kijamii na hata kuzihoji familia na marafiki zao.

Hata hivyo Trump hakueleza nguvu kazi itakayohitajika katika kufanikisha mpango huo. Matamshi yake yanawadia katika wakati mgumu wa kampeini zake, huku anapojaribu kuwashawishi wamarekani kwanini wampigie kura dhidi ya mpinzani wake wa chama cha Democratic Hillary Clinton. Katika hotuba hiyo ya Ohio Trump alionekana kubadili msimamo wake wa awali, wa kuatka kufanyiwa mageuzi muungano wa kijeshi wa Nato na kuapa kushirikiana nao.

Hillary Clinton
Hillary ClintonPicha: picture-alliance/dpa/E. Cromie

"Tutafanya kazi kwa karibu na NATO katika harakati zake mpya za kukabiliana na IS. Awali nikuwa nisema NATO imepitwa na wakati, kwasababu ilishindwa kukabiliana na vilivyo na ugaidi,Tangu nitoe kauli yangu,muungano huo umebadili sera na sasa una kitengo kipya cha kukabiliana na vistisho vya kigaidi.Na jambo nzuri.”amesema Trump.

Taarifa nyingine ni kuwa wafungwa15 waliokuwa wakizuiliwa katika gereza la Guantanamo nchini Marekani wamehamishiwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu, hii ikiwa idadi kubwa ya wafungwa kuhamishwa kwa wakati mmoja mnamo miaka ya hivi karibuni.Uhamisho huo unaifanya idadi ya wafungwa waliosalia katika gereza hilo kuwa 61.Tangu shambulizi la septemba 11, 2011, karibu wafungwa 780 walikuwa wakizuiliwa katika gereza hilo.

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa idara ya serikali 12 miongoni mwa wafungwa hao waliohamishwa ni raia wa Yemen na watatu ni kutoka Afghanistan.Awali wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon ilikuwa imetafuta taifa la tatu kuwapeleka raia hao wa Yemen kutokana na machafuko yanayoendelea katika taifa lao.

Mwandishi: Jane Nyingi/AFPE
Mhariri: Daniel Gakuba