1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: EU ondoeni vizuwizi tutaondoa ushuru

Sekione Kitojo
11 Machi 2018

Rais Trump wa Marekani amerudia madai yake Jumamosi(10.03.2018)kwamba Umoja wa Ulaya usitishe vizuwizi vyake vya biashara kwa biadhaa za Marekani ili kunusuru washirika wake hao na ushuru mpya wa chuma cha pua na bati.

https://p.dw.com/p/2u6oG
USA | Trump in Pennsylvania
Picha: picture-alliance/dpa/AP/C. Kaster

Rais wa  Marekani  amesema  hayo  baada  ya  mazungumzo  magumu mjini  Brussels  kati ya wajumbe  wa  majadiliano  wa  Umoja  wa  Ulaya  na  mwakilishi  wa  masuala  ya biashara  wa Marekani Robert Lighthizer  katika  juhudi za  kumaliza  mzozo  mkubwa ambao  wengi  wanahofia  unaweza  kuingia  katika vita vikubwa  vya  kibiashara.

USA Trump besiegelt Strafzölle auf Stahl und Aluminium
Rais Trump akionesha tamko rasmi la kuongeza ushuru kwa biadhaa za chuma cha pua zitakazoingizwa nchini humoPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Walsh

Afisa  wa  ngazi  ya  juu  wa  biashara  wa  Umoja  wa  Ulaya  amesema  Marekani imeshindwa  kueleza  kwa  uwazi  juu  ya vipi Ulaya  na  Japan zinaweza  kuepuka kodi  hizo zinazotarajiwa  kuanza  wiki  ijayo.

"Umoja  wa  Ulaya , mataifa  safi  kabisa ambayo  yanaitendea  Marekani  vibaya  kabisa katika  biashara, yanalalamika juu  ya  kodi katika  chuma cha  pua na  bati," Trump  alisema.

"Iwapo wataondoa vizuwizi  vyao vibaya kabisa  na  kodi katika  biadhaa  za  Marekani zinazotozwa  hivi  sasa, tutafanya hivyo  hivyo  kuondoa  vyetu. Nakisi  kubwa. Iwapo hawatafanya  hivyo, tutaweka  kodi  kwa  magari. Haki!"

Tangazo la  rais Donald Trump  la  kuweka  ushuru wa  asilimia  25 kwa  chuma  cha  pua kitakachoingizwa  nchini  humo  na  asilimia  10 katika  madini  ya  bati limeuchoma Umoja wa  Ulaya, pamoja  na  washirika  wengine  wakubwa  ikiwa  ni  pamoja  na  Japan, ambayo waziri  wake  wa  uchumi Hiroshige Seko pia  alihudhuria  mazungumzo  hayo  mjini Brussels.

Symbolbild Handelskrieg USA und EU
Ishara ya vita vya kibiashara kati ya Marekani na UlayaPicha: Imago/Ralph Peters

Matarajio ya  EU

"Kama  washirika wakubwa  wa  usalama  wa  Marekani, Umoja  wa  Ulaya  na  Japan wamemsisitizia   balozi Lighthizer matarajio  yao  kwamba   mauzo  ya  nje  ya Umoja  wa Ulaya  na Japan  kwenda  Marekani  yataondolewa katika  kutozwa ushuru  huo mkubwa," taarifa  ya  Umoja  wa  Ulaya  imesema  baada  ya  mazungumzo  hayo.

Lakini baada  ya  mazungumzo  ya  pande mbili  na  Lighthizer, kamishna  wa  biashara  wa Umoja  wa  Ulaya  Cecilia  Malmstroem aliandika  katika  ukurasa  wa  Twitter: "Hakuna maelezo  ya  wazi  juu  ya  utaratibu  hasa  wa  Marekani wa  msamaha  wa  ushuru hata hivyo, kwa  hiyo  majadiliano  yataendelea wiki  ijayo."

Brüssel Japans Wirtschaftminister Seko vor EU-Konsultationen
Waziri wa uchumi wa Japan Hiroshige Seko akiwasili mjini Brussels kwa mazungumzo na mwakilishi wa Marekani na EUPicha: Reuters/F. Walschaerts

Umoja  wa  Ulaya  umekwenda  umbali  zaidi  katika  mapambano  dhidi  ya  hatua  hizo za kushitua  za  Marekani, kwa  kutangaza orodha  ya  bidhaa  za  Marekani  zitakazoathirika  na hatua  za  kulipiza  kisasi iwapo  bidhaa  zake zitaathirika  na  ushuru  huo. Katika  kutangaza hatua  hizo, rais  wa  halmashauri  ya  Umoja  wa  Ulaya  Jean-Claude Juncker alimshambulia Trump, akisema  Umoja  wa  Ulaya  unaweza  kupambana  na "ujinga  kwa  ujinga."

Der Präsident der Europäischen Kommission Jean-Claude Juncker kommt im Regierungsgebäude in Skopje an
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude JunckerPicha: Getty Images/R.Atanasovski

Lighthizer, mfuasi mtiifu  kwa  kauli  mbiu  ya  Trump  ya "Marekani  kwanza" hakutoa  tamko rasmi baada  ya  mazungumzo  hayo, lakini  pande  hizo  tatu  zilikubaliana  kuhusu hatua kadhaa  za  kupambana  na uwepo  wa  bidhaa  nyingi  katika  soko  duniani  kote za chuma cha  pua  na  nyingine, hususan  kutoka  China.

Hatua  hizi  "hazikutarajiwa" na ni chanzo cha  matumaini  ya  tahadhari  kuhusu  kutatuliwa kwa  mzozo  huu  wa  ushuru, amesema  afisa  wa  Umoja  wa  Ulaya  kwa  masharti  ya kutotajwa  jina.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Jacob Safari Bomani