1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kuelekea Vietnam kwa mkutano wa kilele na Kim

Bruce Amani
25 Februari 2019

Rais wa Marekani Donald Trump anaelekea Vietnam kwa ajili ya mkutano wa pili wa kilele na kiongozi wa Korea Kusini Kim Jong Un. Wachambuzi wanahisi kuwa matarajio ya mkutano kati ya viongozi hao wawili yako chini mno

https://p.dw.com/p/3E2AV
US-Präsident Donald Trump und Nordkorea-Präsident Kim Jong Un
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Rais Trump anasema kuwa atakuwa mwenye furaha mradi tu Korea Kaskazini itaendelea kusitisha majaribio yake ya makombora, na kuwa hana haraka ya kusaini mkataba wa nyuklia na kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Un, wakati watapokaa meza moja ya mazungumzo Jumatano na Alhamisi wiki hii.

Mkutano huo wa Hanoi, nchini Vietnam, unakuja miezi minane baada ya mkutano wa kwanza wa kilele na wa kihistoria nchini Singapore, kati ya rais wa Marekani aliyeko madarakani na kiongozi wa Korea Kaskazini.

Viongozi hao wawili waliahidi kufanya kazi ya kuhakikisha kuwa silaha za nyuklia zinaondolewa kabisa katika Rasi ya Korea, lakini makubaliano hayo yasiyo Dhahiri hayajawa na mafikio yoyote muhimu. Maseneta wa chama cha Democratic nchini Marekani na maafisa wa usalama wanamuonya Trump dhidi ya kufikia makubaliano ambayo hayataweza kuzuia mipango ya Korea Kaskazini kutengeneza silage za nyuklia.

Nordkorea Sonderzug von Kim Yong-Un
Kim yuko njiani kueleleka HanoiPicha: picture-alliance/Yonhapnews

Wakati Kim akiwa njiani kuelekea Vietnam kwa mkutano huo akipitia China kwa usafiri wa treni, vyombo vya habari vya Korea Kaskazini vimemuonya Trump kutowasikiliza wakosoaji kutoka Marekani ambao vinasema wanavuruga juhudi za kuimarisha mahusiano.

Akizungumza mjini Washington katika mkesha wa safari yake ya Vietnam, Trump alisema anaamini alionana ana kwa ana na Kim na kuwa walijenga uhusiano mzuri kabisa.

Alisema hana haraka na hataki kumharakisha yeyote, kile asichokitaka tu ni majaribio ya makombora.

Korea kaskazini ilifanya jaribio lake la mwisho la nyuklia, ambalo lilikuwa la sita, mnamo Septemba 2017.

Msemaji mmoja wa rais wa Korea Kusini aliwaambia wanahabari mjini Seoul kuwa pande hizo mbili huenda zikakubaliana kutangaza kumalizika rasmi kwa Vita vya Korea vya 1950 – 1953 katika mkutano huo wa kilele. 

Vita hivyo vilimalizika kwa mapatano ya kusitisha mapigano, lakini sio kwa mkataba na Korea Kaskazini kwa muda mrefu imekuwa ikitoa wito wa kuwepo mkataba wa kuvimaliza rasmi. Pia inataka uhakikisho wa usalama. 

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Mike Pompeo aliliambia shirika la habari la nchini Marekani la Fox News Jumapili kuwa anatumaini hatua kubwa zitapigwa wiki hii lakini Korea Kaskazini haijachukua hatua thabiti za kuwachana na mpango wa nyuklia na kuwa mkutano mwingine wa kilele huenda ukahitajika baada ya ule wa Hanoi.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga