1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa upelelezi kuwasilisha taarifa hiyo

Sylvia Mwehozi
6 Januari 2017

Wakuu wa mashirika ya ujasusi nchini Marekani wanatazamiwa kumkabidhi rais mteule Donald Trump maelezo ya kina juu ya ushahidi walioukusanya kwamba Urusi ilifanya jitihada za kuvuruga uchaguzi wa taifa hilo na udukuzi.

https://p.dw.com/p/2VOPt
USA Präsident Donald Trump
Picha: Getty Images/AFP/D. Emmert

Mkutano huo unakuja wakati kukiwa na mvutano mkali baina ya viongozi wa mashirika ya ujasusi wa Marekani na bosi wao ajaye ambaye amepinga madai yote kwamba Moscow iliingilia uchaguzi huo ili kumsaidia.

Rais Barack Obama ambaye amepokea ushahidi huo amekiambia kituo dada cha utangazaji cha NBC cha Chicago kuwa, "matumaini yangu ni kwamba rais mteule atakapopokea ushahidi huu na akaweza kutathmini uchunguzi, wakati timu yake ikiundwa na wataona namna gani mashirika haya ya kijausi yalivyo na ufanisi na weledi , kwamba baadhi ya mivutano ya sasa itapunguzwa"

Baada ya Trump kuonyesha wasiwasi mapema mwezi uliopita, Obama aliyaamuru mashirika ya ujasusi  kuandaa ripoti ya kina juu ya vita ya mtandaoni na uingiliaji wa Urusi katika uchaguzi. Obama alipelekewa ripoti hiyo jana alhamis na wakuu wa idara ya upelelezi walitegemewa kuitolea maelezo kwa Trump leo ijumaa.

James Clapper
Mkurugenzi wa ujasusi wa taifa wa Marekani James ClapperPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Scott Applewhite

James Clapper , mkurugenzi wa ujasusi wa taifa, Mike Rogers, mkuu wa usalama wa taifa NSA, James Comey, mkuu wa shirika la upelelezi wa ndani FBI na John Brennan mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani CIA walitarajiwa kuhudhuria mkutano huo na bwana Trump.

Clapper ameiambia kamati ya huduma za jeshi katika baraza la seneti jana alhamis kuwa alikuwa anajiamini katika matokeo yake kwamba warusi wamekuwa na historia ndefu ya kuingilia uchaguzi wao na wa watu wengine. "Hii ilikuwa kampeni iliyokuwa na sura nyingi. Kwa hiyo udukuzi ulikuwa sehemu moja tu ya hayo, na pia ulihusisha propaganda za hali ya juu, taarifa na habari za uwongo," alisema Clapper.

Wakuu hao katika kauli yoa ya pamoja wamesema "ni maafisa waandamizi tu wa Urusi" ambao wanaweza kuwa wameruhusu operesheni hiyo ambapo wadukuzi waliiba mafaili ya chama cha Democratic na barua pepe.

Mafaili hayo yalivujishwa kupitia mtandao wa Wikileaks, kukidhoofisha chama na jitihada za Hilary Clinton za kuingia ikulu ya White House.

USA James Comey
James Comey, mkuu wa shirika la upelelezi wa Marekani FBIPicha: picture alliance/AP Photo/J. Scott Applewhite

Makamu wa rais Joe Biden amemshambulia Bw Trump akisema ulikuwa ni wakati kwake kuonyesha ukomavu. Biden anasema "Kua Donald, unapaswa kukua, ni wakati wa kukomaa. Wewe ni rais, unahitaji kufanya jambo. Tuonyeshe ulicho nacho. Utapendekeza sheria , tutahitaji kuzijadili. Acha umma uamue .Wache wapige kura katika bunge ,tuone kitakachotokea."

Trump ambaye ameahidi kutoharibu mahusiano yake na rais Vladmir Putin baada ya kuapishwa rasmi baadae mwezi huu, mara kadhaa amerudia kuyapuuza matokeo ya uchunguzi wao.

Katika siku za nyuma kupitia ukurasa wake wa Twitter, Trump amekejeli makosa ya CIA, FBI na mashirika mengine, akiwapa changamoto ya kuthibitisha kuwa udukuzi na uvujaji unaweza kuunganishwa na serikali ya Putin.

Baadae jana alhamis, aliwauliza tena "kwa jinsi gani na kwanini wako na uhakika juu ya udukuzi", akidai kwamba kamati kuu ya chama cha Democratic ilizuia FBI kupitia seva zake. Trump ameonekana kumuunga mkono mwanzilishi wa Wikileaks Juan Assange na kupendekeza kwamba hata mtoto wa miaka 14 anaweza kuwa amefanya udukuzi huo, suala ambalo limekosolewa na wanasiasa wa vyama vyote.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga