1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki ukingoni mwa kufilisika

Admin.WagnerD30 Juni 2015

Ugiriki inakabiliwa na wakati muhimu sana wakati mpango wake wa kimataifa wa uokozi na washirika wake wa Ulaya ukimalizika pamoja na uwezekano wa kupatiwa msaada mpya wa kuinusuru isifilisike na madeni.

https://p.dw.com/p/1Fq0w
Wananchi wa Ugiriki wakiandamana Athens kupinga mapendekezo ya wakopeshaji. (29.06.2015)
Wananchi wa Ugiriki wakiandamana Athens kupinga mapendekezo ya wakopeshaji. (29.06.2015)Picha: Getty Images/AFP/L. Gouliamaki

Serikali ya Ugiriki inavyoelekea haiwezi kulipa deni lake la euro bilioni 1. 6 kwa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF ambapo muda wa mwisho wa kufanya hivyo ni leo jambo hilo linazidisha hofu kwamba nchi hiyo inaelekea kufilisika vibaya na uwezekano wa kutoka kwenye kanda inayotumia sarafu ya euro barani Ulaya.

Kutokana na kufungwa kwa mabenki na Wagiriki kuwekewa vikomo vya kutowa fedha taslimu zisizozidi euro sitini kwa siku misururu mirefu imekuwa ikionekana nje ya mashine za kutowa fedha benki za ATM. Udhibiti huo wa mitaji umeanza hapo jana na utaendelea takriban kwa wiki moja kufuatia kufungwa kwa mabenki mwishoni mwa juma kulikosababishwa na wito wa Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras kuitisha kura ya maoni juu ya madai ya wakopeshaji ili nchi hiyo iweze kupatiwa mkopo wa kuinusuru.

Tsipras anasema madai ya wakopeshaji ya kutaka nchi hiyo izidi kuchukuwa hatua zaidi za kubana matumizi hayawezi kukubaliwa baada ya kuporomoka kwa uchumi wa nchi hiyo kwa miaka sita.

Wito wa kura ya hapana

Akizungumza katika mahojiano ya televisheni nchini Ugiriki hapo jana wakati maelfu ya wananchi wake wakiandamana katikati ya Athens kuunga mkono kura ya hapana kwa mapendekezo ya wakopeshaji waziri mkuu huyo amewataka wapiga kura wautupilie mpango wao huo.

Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras katika mahojiano ya televisheni nchini Ugiriki. (29.06.2015)
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras katika mahojiano ya televisheni nchini Ugiriki. (29.06.2015)Picha: picture-alliance/AP Photo/T, Stavrakis

Tsipras amekaririwa akisema "Gharama za kiuchumi iwapo kanda ya euro itasambaratika, gharama za nchi kufilisika ambapo Benki Kuu ya Ulaya pekee inaidai zaidi ya euro bilioni 120,maoni yangu binafsi ni kwamba mipango yao sio kuitowa Ugiriki kwenye kanda ya sarafu ya euro,mipango yao ni kufuta matumaini kwamba kunaweza kuwepo na sera aina tafauti barani Ulaya."

Serikali inasisitiza kura ya hapana hapo Jumapili haitomaansiha kutoka kwenye kanda ya sarafu ya euro. Waziri wa Fedha Yanis Varoufakis amekwenda mbali kufikia kutishia kwenda mahakamani iwapo kutakuwepo na majaribio ya kuitowa nchi hiyo kwenye kanda ya sarafu hiyo ya pamoja. Amesema serikali itahakikisha intumia haki zake zote za kisheria.

Makali ya maisha yazidi kupamba moto

Katika mitaa ya Athens Wagiriki wameanza kukabiliana na hali halisi ya mambo ya udhibiti wa fedha taslim. Wastaafu ndio walioathirika zaidi na wanalalamika vikali.

Wagiriki wakiwa nje ya benki iliofungwa mjini Athens.
Wagiriki wakiwa nje ya benki iliofungwa mjini Athens.Picha: Reuters/M. Djurica

Mstaafu mmoja amenukuliwa akitamka kwa hasira "Wale waliosaini kutuangusha kwa sababu yao Alexis Tsipras anashindwa kutafakari mambo vizuri.Halafu kuna wale waliotudanganya.Tuseme hapana kwa wahuni hawa. Bora tufe kwa heshima.Inatosha!"

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wameonya kukataliwa kwa mapendekeozo ya wakopeshaji hapo Jumapili katika kura ya maoni kutapelekea kwa Ugiriki kutoka kwenye kanda ya sarafu ya uero na Umoja Ulaya kwa jumla.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/dpa

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman