1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tuchel aelezea matumaini katika msimu mpya

15 Julai 2016

Borussia Dortmund wamewapoteza wachezaji watatu nyota lakini kocha Thomas Tuchel anasema anataraji kuwa na mwanzo mpya na kuwapa wapinzani wao Bayern Munich ushindani mkali katika msimu mpya

https://p.dw.com/p/1JPeV
Deutschland Mkhitaryan mit Hummels und Gündogan
Picha: Imago/Thomas Bielefeld

Borussia Dortmund walimaliza wa pili katika ligi kuu ya kandanda Ujerumani - Bundesliga na wakafika fainali ya Kombe la Shirikisho la Kandanda Ujerumani - DFB Pokal msimu uliopita lakini kocha Thomas Tuchel anatumai kuwa na mwanzo mpya katika msimu ujao wa Bundesliga wakati kikosi chake kinawakosa wachezaji kadhaa wa zamani nyota.

Tuchel anaendelea na maandalizi ya msimu mpya bila beki Mats Hummels na wachezaji viungo Ilkay Guendogan na Henrikh Mkhitryan, ambao wote waliuzwa mwaka jana.

Lakini Dortmund, baada ya kuwapoteza wachezaji hao, ilijitahidi kuitumia vyema hali hiyo. Klabu ilikusanya zaidi ya euro milioni 100 kutokana na uuzaji wa nyita hao watatu na ikajitosa katika soko la ununuzi wa wachezaji kwa kutumia euro milioni 60.

Beki wa Ureno iliyoshinda Kombe la Ubingwa wa Ulaya 2016, Raphael Guerreiro, beki Marc Bartra, viungo Sebastian Rode, Ousmane Dembele na Mikel Merino, na mshambuliaji Emre Mor wote watajiunga na kikosi hicho wakitaraji kutoa ushindani mkali kwa Bayern ili kuizuia kutwaa taji la tano mfululizo la Bundesliga.

Kikundi cha wachezaji hao waliosajiliwa, ni chipukizi wote na Tuchel anasema anatumai watafanya vyema maana hawakuwa na njia nyingine. Wanaweza kuiga mfano wa Pierre-Emerick Aubameyang na Marco Reus ambao wanafanya vyema katika timu hiyo.

Uli Hoeneß
Rais wa Zamani wa Bayern Uli HoenessPicha: Getty Images/Bongarts/A. Hassenstein

Uli Hoeness kurejea katika nafasi yake Bayern

Na wakati Dortmund wakiendelea kujiimarisha kwa ajili ya msimu mpya, mahasimu wao wakuu Bayern Munich wanaonekana kumrejesha uongozini aliyekuwa rais wa klabu hiyo Uli Hoeness. Baada ya kutumikia kifungo cha miezi 21 jela, Hoeness anarejea katika wadhifa huo, kwa mujibu wa jarida la kandanda la Ujerumani, Kicker.

Hoeness amepewa wadhifa wa heshima wa rais wa klabu, baada ya mkutano wa bodi ya usimamizi, huku mamlaka kamili yakibakia mikononi mwa meneja mkurugenzi Karl-Heinz Rummenigge. Mfanyabiashara na mwanauchumi Karl Hopfner mwenye umri wa miaka 63 amekuwa akishikilia wadhifa huo wa rais wa Bayern Munich tangu Machi 2014 wakati Hoeness alifungwa jela, lakini kila mara alisisitiza kuwa atajiuzulu mara baada ya mtangulizi wake ataondoka jela. Hoeness aliachiwa huru kutoka gereza la Landsberg mwishoni mwa Februari baada ya kuhukumiwa Machi 2014 kwa kukwepa kulipa karibu euro milioni 28.5 za kodi kutoka kwa kampuni yake ya kuuza soseji na nyama.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Iddi Ssessanga