1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya ufisadi Myanmar yamshtaki Suu Kyi

Tatu Karema
10 Juni 2021

Tume ya kupambana na rushwa nchini Myanmar, imegundua kwamba aliyekuwa kiongozi Aung San Suu Kyi alikubali rushwa na kutumia vibaya mamlaka yake kupata faida kupitia mikataba katika sekta ya mali isiyohamishika

https://p.dw.com/p/3ugsu
Myanma State Counsellor Aung San Suu Kyi
Picha: Athit Perawongmetha/REUTERS

Mawakili wa Suu Kyi tayari walikuwa wamekanusha madai hayo wakati yalipotajwa kwa mara ya kwanza miezi mitatu iliyopita na uongozi wa jeshi la nchi hiyo ambao uliipindua serikali yake iliyochaguliwa kikatiba mnamo mwezi Februari. Haya yanajiri huku upande wa mashtaka ukijiandaa kuwasilisha mashtaka mengine dhidi ya Suu Kyi katika mahakama siku ya Jumatatu.

Wafuasi wa Suu Kyi wanasema kuwa mashtaka yote yamechochewa kisiasa na ni jaribio la kumdhalilisha na kuhalalisha hatua ya jeshi ya kutwaa mamlaka. Hatua hiyo ya jeshi, imeshtumiwa vikali na raia wengi wa nchi hiyo waliokipigia kura kwa wingi chama cha National League for Democracy kinachoongozwa na Suu Kyi katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana baada ya kuwa uongozini kwa miaka mitano . Iwapo atapatikana na hatia, Suu Kyi atapigwa marufuku kushiriki katika uchaguzi ujao iwapo utaandaliwa. Uongozi wa jeshi nchini humo, umesema kuwa utaandaa uchaguzi mpya katika muda wa mwaka mmoja au miwili ijayo lakini jeshi hilo lina historia ya kuahidi kuhusu chaguzi bila kutimiza ahadi hizo.

Straßenschlachten in Myanmar
Jeshi la MyanmarPicha: AFP/Getty Images

Wakati huo huo, taarifa iliyotolewa na Min Tun imesema kuwa ndege iliyokuwa imewabeba wafanyakazi sita na abiria wanane, imeanguka karibu na mji wa Pyin Oo lwin hii leo na kusema ajali hiyo ilisababishwa na hali mbaya ya hewa. Taarifa hiyo imeongeza kwamba ndege hiyo ilipoteza mawasiliano ilipokuwa umbali wa futi 1300 kutoka kiwanda kimoja cha chuma karibu na uwanja wa ndege.

Taarifa hiyo imesema kuwa mtawa mmoja alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wameabiri ndege hiyo na kuongeza kuwa kundi la waokoaji limefanikiwa kumuokoa mvulana mmoja na afisa mmoja wa jeshi aliyekuwa ametumwa katika hospitali ya kijeshi iliyoko karibu. Ajali za ndege ni jambo la kawaida nchini Myanmar kutokana na sekta ya usafiri wa ndege ambayo haijaimarika huku msimu wa masika ukisababisha matatizo kwa ndege za kibiashara na kijeshi katika siku zilizopita.

Ndege moja ya kijeshi ilianguka katika bahari ya Andaman mnamo mwaka 2017 na kuwauwa watu wote 122 waliokuwa wameiabiri hiyo ikiwa moja ya ajali mbaya zaidi katika sekta hiyo ya uchukuzi wa ndege katika historia ya nchi hiyo. Baadaye maafisa wa serikali walisema ilisababishwa na hali mbaya ya hewa.