1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya Umoja wa Mataifa inayochunguza uvamizi wa meli ya misaada yaanza kazi leo

Josephat Nyiro Charo10 Agosti 2010

Masuala nyeti yanatakiwa kutilia maanani kuwezesha uchunguzi huo kuleta tija. Uturuki italazimika kujibu maswali magumu kwa nini haikusikiliza ushauri wa Israel na ikiwa wanaharakati walikuwa na silaha

https://p.dw.com/p/Ogba
Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akishuhudia mbele ya jopo la kitaifaPicha: AP

Siku moja baada ya waziri mkuu wa Israel kutoa ushahidi mbele ya jopo la kitaifa la Israel linalochunguza uvamizi wa msafara wa meli za misaada zilizokuwa zikielekea Ukanda wa Gaza mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, hii leo mjini New Marekani kunaanza uchunguzi wa kimataifa kuhusu mkasa huo ambapo wanaharakati tisa wa Kituruki waliuwawa, mmoja wao akiwa pia Mmarekani.

Ukweli halisi wa mambo hauwezi kupingika: Mnamo tarehe 31 mwezi Mei mwaka huu, wanajeshi wa majini wa Israel waliivamia meli ya misaada ya Kituruki kwa jina Mavi Marmara na kuwaua wanaharakati tisa wanaowaunga mkono Wapalestina kwenye eneo la bahari lililo nje ya mpaka wa Israel. Kulizuka ghadhabu na mvutano ikiwa Waturuki tisa waliouwawa walikuwa kweli wanaharakati wa kutoa misaada ya kibinadamu au walikuwa wanamgambo.

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye jana alitoa ushahidi mbele ya jopo maalum la Israel linalochunguza kisa hicho, alisema wakati huo kwamba wanajeshi wa Israel walihitaji kujilinda.

"Walianza wao kuwashambulia wanajeshi wetu wa kwanza waliongia ndani ya meli. Wanajeshi wetu walipigwa, kukanyagwa na hata risasi zilifyetuliwa. Walihitaji kujilinda vinginevyo wangeuwawa wao. "

Lakini waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayip Erdogan, alioyaona matamshi ya waziri mkuu Netanyahu kuwa si sahihi. Baada ya uvamizi huo alizungumzia wazi kuhusu ugaidi wa taifa la Israel na kutaka ichukuliwe hatua kali.

"Mauaji haya ya umwagaji damu ambayo Israel imefanya dhidi ya msafara wa meli za misaada, lazima yaadhibiwe vikali. Huo ulikuwa uvamizi dhidi ya haki za kimataifa, ubinadamu na amani ya dunia. "

Tayyip Erdogan
Waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip ErdoganPicha: AP

Tume maalum ya Umoja wa Mataifa ambayo inaanza rasmi kufanya kazi yake hii leo mjini New York, Marekani, yenyewe haina uwezo wa kuiadhibu Israel. Inatakiwa kufafanua, kutoa mapendekezo na kuchunguza ushahidi wa picha na kanda za video, ambazo wafuasi na wapinzani wa msafara wa meli za misaada walizituma kwenye tovuti za kijamii za facebook na Youtube kwenye mtandao wa intaneti. Israel na Uturuki zimeruhusiwa kupeleka wajumbe wao kwenye tume hiyo, jambo ambalo huenda likapunguza uwezekano wa kupatikana ufanisi katika uchunguzi huo.

Awali Israel ilikataa katakata miito ya Umoja wa Mataifa, Marekani na nchi za Ulaya kama vile Ujerumani, ikubali uchunguzi wa kimataifa. Waziri wa mambo ya kigeni wa Israel, Avigdor Lieberman, alikuwa na msimamo mkali kuhusu suala hilo na kueleza.

"Jambo la kwanza muhimu kwangu ni afadhali kulazimika kubeba lawama za jumuiya ya kimataifa, badala ya kuwazika wanajeshi wetu. Pili, msafara wa meli za misaada haukufika Gaza na hakuna meli yoyote itakayofika katika pwani ya Gaza."

Israel AußenMinister Avigdor Lieberman
Waziri wa mambo ya kigeni wa Israel, Avigdor LiebermanPicha: AP

Ingawa Israel safari hii imekubali uchunguzi wa kimataifa, ikilinganishwa na matukio mengine ya awali, kuna hoja mbalimbali za kuzingatiwa. Muundo wa tume ya Umoja wa Mataifa inaongozwa na mtu asiyeegemea upande wowote: kiongozi wa serikali ya Newzealand, Geoffrey Palmer. Kutakuwa pia na wajumbe wa Isreal na Uturuki na rais wa zamani wa Colombia, Alvaro Uribe, ambaye anatajwa kuipendelea Israel. Kwa upande mwingine, Israel inashinikiza kwamba tume hiyo isiruhusiwe kuwahoji moja kwa moja wanajeshi wake.

Vyombo kadhaa vya habari nchini Israel viliripoti kwamba wanajeshi wa Israel walitumia nguvu kupita kiasi katika kuivamia meli hiyo ya misaada. Taarifa zilizonea mbali ni kwamba wanajeshi wa Israel walilazimika kujilinda. Uturuki bila shaka italazimika kujibu maswali magumu kwa mfano: Je wanaharakati walikuwa wamejihami na silaha? Na kwa nini meli hiyo ilivuka mpaka hata baada ya Israel kuonya ingeishambulia kama ingevunja kuzingirwa kwa Ukanda wa Gaza kwa upande wa baharini?

Kwa ujumla, kuna tume tano zinazochunguza mauaji hayo kwenye meli ya Mavi Marmara. Kuna tume ya Umoja wa Mataifa,mjini New York, Marekani, jopo la baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi, na majopo yaliyoundwa na wanasiasa na majopo ya kijeshi. Ikiwa kweli uchunguzi wa mvutano huu wenye hamasa kubwa ya kisiasa utaleta tija, ni jambo la kusubiri na kuona.

Mwandishi:Sollich, Rainer (DW Arabisch)/ZPR/Charo,Josephat

Mhariri: Othman Miraji