1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tunisia: Rais Kais Saied amfuta kazi Waziri Mkuu

Zainab Aziz Mhariri: Jacob Safari
26 Julai 2021

Nchini Tunisia Rais Kais Saied amemfukuza kazi Waziri wake Mkuu Hicham Mechichi. Rais huyo wa Tunisia amechukua hatua hiyo baada ya kufanyika maandamano yaliyogeuka na kuwa ghasia.

https://p.dw.com/p/3y3s2
Tunesien Präsident Kais Saied
Picha: picture-alliance/Photoshot/Handout Tunisian Presidency

Rais Saied alitoa taarifa juu ya hatua aliyochukua ya kumfukuza waziri wake mkuu Hicham Mechichi baada ya kufanyika kikao cha dharura kwenye ikulu. Leo hii rais wa Tunisia amemteua Khaled Yahyaoui, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa kitengo cha usalama wa rais, kusimamia Wizara ya Mambo ya Ndani.

Rais wa Tunisia pia amesimamisha shughuli za bunge kwa siku 30. Kwa mujibu wa taarifa, hayo yametokea baada ya maandamano yaliyosababisha vurugu. Waandmaanaji walikuwa wanapinga vizuizi vya kupambana na corona na pia hali mbaya ya uchumi nchini Tunisia. Hatua nyingine iliyochukuliwa na rais Kais Saied ilikuwa ni kuwaondolea kinga wabunge wote. Amesema atamtangaza waziri mkuu mpya katika saa chache zijazo ili kuleta utulivu nchini.

Waziri Mkuu wa Tunisia aliyeondolewa madarakani Hichem Mechichi
Waziri Mkuu wa Tunisia aliyeondolewa madarakani Hichem MechichiPicha: Hassene Dridi/AP Photo/picture alliance

Kiongozi huyo wa Tunisia ametumia kipengele maalum cha katiba kinachomruhusu kuchukua madaraka ya kiutendaji na kulifunga bunge kwa kipindi kisichojulikana hadi wakati ambapo utendaji wa kawaida wa taasisi zote utakaporejeshwa.

Ingawa rais Saied amesisitiza kuwa hatua yake ilikuwa ya kikatiba, Spika wa Bunge Rached Ghannouchi amemshutumu rais huyo kuwa alichokifanya ni mapinduzi dhidi ya harakati za mapinduzi nchini Tunisia na katiba ya nchi hiyo. Rais Saied amedai kuwa chini ya Ibara ya 80 ya katiba ya nchi hiyo anaruhusiwa kuchukua hatua kama hiyo ikiwa kuna hatari. Amesema katiba hairuhusu kuvunjwa kwa bunge, lakini inaruhusu kusimamisha shughuli zake.

Watunisia wanaoziunga mkono pande zinazopingana mapema leo walijazana nje ya majengo ya bunge na kuanza kurushiana mawe ambapo baadhi ya watu wameripotiwa kujeruhiwa. Kulingana na shirika la habari la AFP polisi waliwakamata waandamanaji kadhaa na walilazimika kutumia gesi ya kutoa machozi wakati umati huo ulipokuwa ukirushiana mawe.

Waandamanaji wafuasi wa chama cha Ennahda katika jiji la Tunis nchini Tunisia
Waandamanaji wafuasi wa chama cha Ennahda katika jiji la Tunis nchini TunisiaPicha: Yassine Gaidi/AA/picture alliance

Tunisia inakabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi katika kipindi cha muongo mmoja kuhusiana na swala la demokrasia baada ya Rais Kais Saied kumwondoa madarakani waziri mkuu Hichem Mechichi na kulizuia bunge katika hatua ambayo inaonekana kuungwa mkono na jeshi lakini inapingwa na kuitwa kuwa ni mapinduzi na wapinzani wakiwemo viongozi wa Kiislam wenye ushawishi mkubwa.

Yote haya yanatokea baada ya miezi kadhaa ya mizozo kati ya rais Kais Saied na Waziri Mkuu Hichem Mechichi na pia bunge lililogawanyika. Tunisia pia imetumbukia zaidi kwenye mgogoro wa kiuchumi unaozidishwa na janga la COVID-19.

Rais wa Tunisia Kais Saied.
Rais wa Tunisia Kais Saied.Picha: Fethi Belaid/AFP/Getty Images

Matatizo ya muda mrefu yanayotokana na ukosefu wa ajira pamoja na kudorora kwa utendaji kazi wa serikali ndiyo masuala yaliyochochea maandamano ya kuipinga serikali nchini Tunisia. Pamoja na nakisi katika bajeti,Tunisia inakabiliwa na matatizo ya kulipa madeni yake. Huenda nchi hiyo ikalamizika kutafuta mkopo mwingine kutoka shirika la fedha la IMF ambao unaweza kutifua matatizo mengine.

Vyanzo:/RTRE/AP/ https://p.dw.com/p/3y2IC