1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tusk aibuka mshindi uchaguzi Poland

16 Oktoba 2023

Vyama vya upinzani nchini Poland vilivyoahidi mfumo wa kikatiba kuendana na viwango vya Umoja wa Ulaya vinaelekea kushinda wingi wa viti bungeni kuhitimisha miaka minane ya utawala wa chama cha Sheria na Haki (PiS).

https://p.dw.com/p/4XbCw
Polen Krakau | Flaggen Polen & EU, Anhänger der Opposition
Alama ya bendera ya Poland na Umoja wa Ulaya, ishara ya vyama vya upinzani nchini Poland.Picha: Beata Zawrzel/NurPhoto/picture alliance

Matokeo ya awali yalionesha kuwa Muungano wa Kiraia wa rais wa zamani wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Donald Tusk, ulikuwa umeshinda viti 163 katika bunge lenye jumla ya viti 460, na vyama viwili vidogo vya Third Way na cha mrengo wa Kushoto vimepata viti 55 na 30 mtawalia.

Matokeo haya ya awali yanavipa vyama hivyo vitatu wingi wa jumla ya viti 248 huku chama cha PiS kikitazamiwa kupata viti 200 na chama cha mrengo mkali wa kulia cha Confederation, chenye uwezekano wa kushirikiana na PiS, kikitabiriwa kupata viti 12 tu. 

Soma zaidi: Matumaini ya EU baada ya uchaguzi wa Poland

Uchaguzi wa Jumapili (Oktoba 15) ulishuhudia ushiriki mkubwa zaidi wa wapiga kura, ukipita hata uchaguzi wa kwanza huru baada ya kuanguka kwa Ukomunisti.

Tusk alitangaza ushindi baada ya kuanza kutolewa kwa matokeo ya awali, na kusema demokrasia imeshinda.

"Matokeo haya yanajieleza yenyewe. Hakuna anaeweza kuyabadilisha, hakuna anayeweza kutunyang'anya ushindi huu, tumeshinda demokrasia, tumeshinda uhuru, tumeirejesha Poland yetu. Tutaunda serikali haraka iwezekanavyo, serikali nzuri ya kidemokrasia na washirika wetu. Poland imeshinda, mmeshinda, wanaume na wanawake wa Poland wameshinda." Alisema mkuu huyo wa zamani wa Umoja wa Ulaya.

Tusk arejea madarakani

Tusk, mwenye umri wa miaka 66, alihudumu kama Waziri Mkuu wa Poland kati ya 2007 na 2014 na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya kati ya 2014 na 2019.

Polen | Parlamentswahl | Donald Tusk beim Wahlabend der KO
Muungano unaongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Poland, Donald Tusk, amefanikiwa kupata wingi wa viti bungeni.Picha: Kacper Pempel/REUTERS

Kiongozi huyo aliahidi kurejesha uhusiano mzuri na Umoja wa Ulaya na kufungua ufadhili uliozuiliwa kwa sababu ya mabishano katika miaka minane ya serikali ya PiS.

Soma zaidi:Raia wa Poland washiriki katika uchaguzi wa bunge 

Vile vile aliahidi kuhalalisha utoaji mimba - suala kuu la mzozo dhidi ya serikali ambayo inasisitiza maadili ya jadi ya Kikatoliki. 

Kiongozi wa chama cha PiS, Jaroslaw Kaczynski, mwanasiasa wa siku nyingi mwenye umri wa miaka 74, ambaye kaka yake Lech  Kaczynski alikufa katika ajali ya ndege mwaka 2010 akiwa rais, amesema bado ana matumaini kwamba chama chake kinaweza kuunda serikali.

"Tutafanya kila kinachowezekana kuhakikisha kuwa mpango wetu unaendelea kutekelezwa licha ya muungano unaotupinga." Alisema.

Kiza kirefu mbele

Hata hivyo, mchambuzi wa kisiasa Stanislaw Mocek, kutoka taasisi ya Collegium Cavitas, alisema anaamini huu ndio mwisho wa serikali ya PiS.

Naye Michal Baranowski, mchambuzi kutoka taasisi ya Marshall Fund ya Ujerumani, alisema Poland inaweza kurejea kwenye nafasi ya maamuzi ya Umoja wa Ulaya, akifafanuwa kuwa matokeo ya awali yanaashiria kuundwa kwa serikali imara.

Wachambuzi pia wameonya kuwa serikali yoyote ya muungano itakayoundwa na upinzani huenda ikakabiliwa na mivutano ya mara kwa mara na Rais Andrzej Duda, ambaye ni mshirika wa chama cha PiS.