1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tuzo mbadala ya Nobel yatunukiwa Wasaudi Arabia

Saumu Mwasimba
24 Septemba 2018

Wanaharakati watatu wa haki za binadamu kutoka Saudia walioko jela watunukiwa tuzo mbadala ya Nobel na taasisi ya Nobel mjini Stockholm. Pia wapinga rushwa kutoka Guatemala watunukiwa tuzo ya heshima

https://p.dw.com/p/35OIy
***SPERRFRIST 24.09.2018 um 09.00 Uhr*****  Right Livelihood Award Abdullah al-Hamid, Mohammad Fahad al-Qahtani und Waleed Abu al-Khair
Picha: Right Livelihood Award/Ahmed al-Osaimi

Washindi wa tuzo maalum ya haki za binadamu au tuzo mbadala ya Nobel wametangazwa leo hii mjini Stockholm Sweden. Tuzo hiyo imetunukiwa watetezi watatu wa haki za binadamu wakisaudi waliofungwa jela pamoja na wanaharakati wa kupinga rushwa kutoka Amerika Kusini.

Taasisi ya tuzo hiyo mjini Stolkholm imesema dolla 113,400 zinazoambatana na tuzo hiyo mbadala ya Nobel zitagawanywa kwa washindi Abdullah al Hamid,Mohammad al-Qahtani na Waleed Abu al Khair wote wa Saudi Arabia kutokana na juhudi zao za kijasiri zinazosimamia misingi ya haki za binadamu ya kimataifa,ili kuleta mageuzi katika mfumo wa kidhalimu wa kisiasa nchini Saudi Arabia.

Tuzo  ya heshima ya mwaka huu imetunukiwa Thelma Aldana wa Guatemala na mkolombia Ivan Velasquez kutokana na mchango wao mkubwa katika kuyafichua matumizi mabaya ya mamlaka pamoja na uozo wa rushwa.

***SPERRFRIST 24.09.2018 um 09.00 Uhr*****  Right Livelihood Award Bildkombo Ivan Velasques und Thelma Aldana
Ivan Velasques na Thelma AldanaPicha: Getty Images/AFP/O. Estrada//J. Ordonez

Tuzo ya Right Livelihood ambayo pia inajulikana kama tuzo mbadala ya Nobel ni tuzo inayotolewa kila mwaka  tangu ilipoanzishwa mwaka 1980 na mwanahisani Jakob von Uexkull raia wa Sweden mwenye asili ya Kijerumani kwa lengo la kuwatunuku watu wanaoendesha juhudi ya kupigania haki za binadamu duniani wanaohisiwa kupuuzwa au kutopewa nafasi katika tuzo za Nobel. Al Qahtani na Al-Hamid ni wanaharakati waasisi wa chama cha kupigania haki za kiraia na kisiasa nchini Saudi Arabia kinachojulikana kwa kiarabu kama HASEM.

Mwaka 2013 walihukumiwa kufungwa jela miaka 10 na 11 mtawalia na punde baada ya wanaharakati hao kuhukumiwa wanaharakati wengine kadhaa nao walifuatia kufungwa. Hukumu zote hizo zilikuja katika kipindi cha kuzuka wimbi la harakati za kupigania mageuzi katika nchi za kiarabu mwaka 2011.

Serikali ya Saudi Arabia haikutowa jibu mara moja pale ilipoombwa na shirika la habari la Associated Press kutoa kauli kuhusu tuzo hizo zilizotangazwa leo. Wanaharakati wa Amerika ya Kusini waliotunukiwa pia tuzo hiyo Aldana na Velasquez wote wawili waliwahi kuwa waendesha mashtaka wakuu na pia waliwahi kuwa wakuu wa tume ya kimataifa dhidi ya ukwepaji mkono wa sheria nchini Guatemala iliyojulikana kama CICIG.

Ikumbukwe kwamba hata katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amekataa ombi la Guatemala la kumtaka achague mkuu mpya wa CICIG akisema haoni sababu yoyote ya kumbadilisha mkuu wa sasa wa tume hiyo Velasquez. CICIG ni tume huru iliyopewa jukumu tangu 2006 na Umoja wa Mataifa kuwaandamana wahalifu wakubwa nchini Guatemala.

Guatemala | Generalstaatsanwältin Thelma Aldana und  UN-Kommissar Ivan Velasquez
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Castillo

Thelma Aldana amesema kupitia taarifa iliyotolewa na taasisi ya Tuzo hiyo mjini Stolkholm kwamba -tuzo mbadala ya Nobel ambayo atakabidhiwa Novemba 23 mjini Stolkholm ni hatua ya kutambua mapambano na harakati za watu wa Guatemala dhidi ya rushwa, kauli ambayo pia inafanana na ile iliotolewa na mwenzake, Ivan Velasquez aliyeongeza kusema kwamba ni tuzo muhimu kwao kwa sababu itayafungua macho ya walimwengu katika kuimulika Guatemala.

Tuzo ya pili imetolewa kwa Yacouba Sawadogo  wa Burkina Faso kutokana na juhudi zake za kuibadili ardhi ya jangwa kuwa msitu hatua ambayo imechangia kusaidia wakulima kupata rutuba tena katika ardhi zao.

Tuzo ya tatu imetunukiwa mtaalamu wa masuala ya kilimo kutoka Australia Tony Rinaudo ambaye ameonesha mfano mkubwa kuhusu jinsi ardhi kavu inavyoweza kugeuzwa kuwa ya kilimo kwa gharama ndogo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/ AP /Daniel Heinrich (DW)

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman