1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uamuzi wa Harry na mkewe Meghan waumiza familia ya kifalme

Sylvia Mwehozi
9 Januari 2020

Mwanamfalme wa Uingereza, Harry na mkewe Meghan wametangaza kuachana na majukumu yao ya ngazi ya juu katika familia ya kifalme. Wanandoa hao pia wamesema wanapanga kutumia muda wao mwingi Amerika ya Kaskazini.

https://p.dw.com/p/3Vvc9
UK Monarchie l Prinz Harry und Herzogin Meghan
Picha: picture-alliance/AP/M. Dunham

Taarifa iliyotolewa na kasri la Buckingham imeeleza kuwa Harry na Meghan wataendelea kumuunga mkono kikamilifu Malkia Elizabeth. Wamebainisha kuwa wanataka pia kujitegemea kifedha.

"Baada ya miezi mingi ya kutafakari na majadiliano ya ndani, tumeamua kufanya mabadiliko mwaka huu kwa kuanza kutekeleza jukumu jipya ndani ya taasisi hii", alisema Harry ambaye yuko nafasi ya sita katika orodha ya warithi wa kiti cha Ufalme. Wanandoa hao wamesema watawasilisha maelezo kamili juu ya "hatua yao inayofuata" mapema inavyowezekana, wakati wakijadiliana na Malkia Elizabeth, na baba yake Harry Mwanamfalme Charles na William ambaye ni kaka yake.

UK Monarchie l Prinz Harry und Herzogin Meghan
Meghan na mumuwe HarryPicha: picture-alliance/dpa/PA/T. Melville

Hata hivyo muda wa maamuzi yao unaonekana kuwashangaza wanafamilia wa kifalme, akiwemo Malkia mwenyewe, kulingana na chanzo kimoja ndani ya familia hiyo. "Ndugu wengine wa familia hawakuhusishwa juu ya hili", kilisema chanzo hicho kilichozungumza na Reuters.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya makao makuu ya Malkia Elizabeth, mazungumzo yanaendelea kati ya mwanamfalme Harry na mkewe kuhusu mipango yao hiyo. Kasri hilo limesema kuwa wanaelewa kuhusu nia yao, lakini masuala hayo kwa sasa ni magumu na itachukua muda kuyafanyia kazi na kwamba mazungumzo yako katika hatua za awali.

Taarifa zaidi zinasema familia ya Kifalme imeumizwa na kufadhaishwa na tangazo la kushutusha la Harry na mkewe. Harry mwenye miaka 35 na Meghan mwenye miaka 38 na mtalaka ambaye mama yake ni Mmarekani mweusi walioana mwaka 2018 katika sherehe zilizofanyika kasri la Windsor. Mwaka jana walifanikiwa kupata mtoto wao wa kwanza wa kiume Archie Harrison Mountbatten-Windsor.