1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubalozi wa Israel nchini Misri, washambuliwa

Halima Nyanza(ZPR)10 Septemba 2011

Waziri Mkuu wa Misri ameitisha kikao cha dharura cha baraza la mawaziri baada ya waandamanaji kuushambulia ubalozi wa Israel mjini Cairo jana usiku na kutupa mamia ya nyaraka za ubalozi huo.

https://p.dw.com/p/12WUa
Waandamanaji nchini MisriPicha: dapd

Balozi wa Israel nchini Misri ameripotiwa kuondoka nchini humo mapema leo, kurejea nyumbani.

Rais Barack Obama wa Marekani ameitaka Misri kuulinda ubalozi huo dhidi ya waandamanaji na katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ameeleza wasiwasi wake kuhusu tukio hilo.

Mamia ya polisi na wanajeshi wamepambana na waandamanaji ambao jana usiku, waliuvunja uzio unaozunguka jengo la ubalozi wa Israel mjini Cairo. Uzio huo ulijengwa na serikali ya Misri baada ya maandamano kufanywa kila siku nje ya ubalozi wa Israel, kupinga mauaji ya walinzi watano wa mpakani wa Misri, katika mji wa Sinai.

Erneute Gewalt zwischen Israel und Palästinensern August 2011
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, akimjulia hali mmoja wa majeruhi katika ghasia zilizotokea mpakani mwa nchi hiyo na MisriPicha: dapd

Walinzi hao waliuawa kwenye mpaka wa Misri, katika shambulio la Israel lililowalenga wapiganaji wa Kipalestina.

Kufuatia ghasia hizo za waandamanaji mjini Cairo, Misri imetangaza tahadhari ya hali ya juu.