1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubelgiji yafungua tena 'Makumbusho ya Afrika' yenye utata

Daniel Gakuba
9 Desemba 2018

Jumba la Makumbusho linalohifadhi sana iliyoporwa Afrika wakati wa ukoloni limefunguliwa tena karibu na Brussels baada ya kukarabatiwa. Maafisa wake wanasema jumba hilo sasa limejaribu kubadilisha mtazamo wa kikoloni.

https://p.dw.com/p/39lV9
Belgien Königliches Museum für Zentral-Afrika
Picha: DW/W. Bashi

Jumba hilo la makumbusho lililo katika mji mdogo wa Tervuren karibu na Brussels, ambalo siku za nyuma lilikosolewa vikali kutukuza ukoloni wa Mbelgiji na unyama wake dhidi ya wenyeji wa nchi zilizotawaliwa na nchiyo, lilifungua tena milango yake Jumamosi (08.12.2018) baada ya miaka 5 ya kazi za kulikarabati.

Kuanzishwa kwa makumbusho hayo kulitokana na wazo la Mfalme Leopold II wa Ubelgiji mwanzoni mwa karne ya 20, na yalihifadhi vitu vilivyokusanywa kutoka katika makoloni ya Ubelgiji, ambayo kwa majina ya leo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Rwanda.

Mfalme Leopold aliitawala Kongo kama shamba lake binafsi, akiendesha unyonyaji wa mali asili za nchi hiyo, na kuwafanyisha kazi za shuruti wenyeji kwa ukatili wa kupindukia, ambao unakisia kuwauwa watu milioni 10 kupitia kazi ngumu, vipigo na magonjwa.

Slideshow zur Belgischen Kolonialvergangenheit Congo Belge Flash-Galerie
Awali makumbusho haya yaliutukuza ukoloni wa kibelgiji kama juhudi za kuleta ustaarabu kwa Waafrika, yalikifumbia macho uovu wa utawala huo.Picha: Royal Museum for Central Africa Tervuren

Katika hali yake ya awali, Makumbusho hayo ya Afrika yaliwatukuza maafisa wa kikoloni, na Waafrika hawakuwakilishwa kana kwamba eneo lililotawaliwa halikuwa na watu. Wabelgiji wengi wa sasa hawana uelewa kuhusu maovu yaliyotendwa na nchi yao kwa nchi ilizozitawala kikoloni, kwa sababu historia yake haifundishwi mashuleni, na yamekuwa yakifunikwafunikwa na makumbusho kama haya.

Mabadiliko ya kimtazamo

Baada ya kukarabatiwa, eneo la makumbusho hayo hivi sasa lina ukubwa wa mita 11,000 za mraba, na ukarabati huo umegharimu kiasi cha dola 74 milioni. Miongoni mwa vyumba vya maonyesho, vipo sasa vinavyojikita juu ya ukoloni wa Wabelgiji nchini Kongo, ambao ulimalizika mwaka 1960.

Lakini,mkurugenzi wake mkuu Guido Gryseels anasema mara hii makumbusho haya yanachukua mtazamo wa Afrika ya sasa, na ni chumba kimoja tu ambacho kimetengwa maalum kwa ajili ya kumbukumbu ya kipindi cha ukoloni.

Königliches Museum für Zentralafrika in Tervuren
Marekebisho yaliyofanywa ni pamoja na kuyapa makumbusho haya sura ya kiafrikaPicha: DW/T. Schultz

Ipo sehemu ya mbinu za kisasa za kumbukumbu inayotumia picha na vidio, ambapo Wakongo, Warundi na Wanyarwanda wanaonekana na kusikika wakielezea hali zao.

Vile vile, tofauti na siku za nyuma, anasema Gryseels, makumbusho hayo yanajitahidi kuwaajiri watu wenye asili ya Afrika, ambao wameanza kuwa sehemu ya jamii ya Ubelgiji. Miongoni wa kazi za sanaa za za sasa, zimetengenezwa na watu kutoka nchi zilizokuwa makoloni ya Ubelgiji.

Utata juu ya umiliki wa kumbukumbu

Kufunguliwa upya kwa makumbusho haya kumefanyika wakati kukiwa na miito ya kutaka kazi za sanaa na vitu vingine vya kumbukumbu vilivyochukuliwa kimabavu na wakoloni kutoka Afrika, virudishwe katika nchi vilikotoka.

Mwezi uliopita Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alisema haikubaliki kwamba asilimia 90 ya sanaa ya Afrika inapatikana nje ya bara hilo, na kuongeza kwamba kimsingi, inabidi majumba ya makumbusho barani Ulaya yarejeshe vitu hivyo.

Paris - Ausstellung Beauté Congo
Asilimia 90 ya kazi za sanaa ya kiafrika ziko nje ya Afrika Picha: Pilipili Mulongoy

Guido Gryseels wa Makumbusho ya Tervuren anakubaliana na Rais Macron kwamba vitu walivyo navyo ni utambulisho wa Waafrika, na ni mali yao, lakini anasema kulingana na hali halisi, yapo mengi ya kujadiliwa.

Mmoja wa maafisa wakuu wa makumbusho hayo anasema kwa hali ya sasa, maslahi ya Afrika yanazingatiwa kwa kiasi fulani, kwa sababu angalau sasa sura za waafrika zinaonekana, tofauti na awali ambapo makumbusho hayo yaliwakilisha nchi na kuwapuuza watu wake, na kuwanyima utu wao.

Wasi wasi juu ya uwezo wa miundombinu Afrika

Baadhi ya wataalam wa masuala ya makumbusho wanaelezea wasiwasi wao, kwa hoja kwamba vitu vilivyo katika makumbusho ya Ulaya vinaweza kuharibika vikirudishwa Afrika, kwa sababu baadhi ya nchi vilikotoka, kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo havina hata makumbusho ya kitaifa.

Eröffnung Musée des Civilisations noires MCN in Senegal
Makumbusho ya Ustaarabu wa Mtu Mweusi mjini Dakar, SenegalPicha: AFP/Getty Images/Seyllou

Mkurugenzi Guido Gryseels ameiambia idhaa hii kwamba wanafanya mazungumzo na serikali ya Rwanda, ya kuyaweka katika mfumo wa kidijitali maandishi, picha, sauti na vidio vyote vilivyochukuliwa na wakoloni wa kibelgiji, na kuvirusha katika makumbusho ya taifa ya Rwanda.

Kuna hatua inayopigwa barani Afrika katika sekta ya makumbusho ya kale. Wiki hii Senegal ilifungua mjini Dakar makumbusho ya kisasa yajulikanayo kama ''Makumbusho ya Ustaarabu wa Watu Weusi'', kama mwanzo wa mfululizo wa mengine yatakayojengwa katika nchi mbali mbali za kiafrika. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa ushirikiano na Ubelgiji, inajenga pia makumbusho ya kitaifa mjini Kinshasa.

Mwandishi: Daniel Gakuba

Mhariri:Yusuf Saumu