1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UBINGWA WA RIADHA DUNIANI

Mohamed Dahman22 Agosti 2009
https://p.dw.com/p/JGVH
Abel Kirui wa Kenya akifurahia wakati akivuka mstari wa ushindi katika mbio za marathon leo hii mjini Berlin.Picha: AP

      Abel Kirui mwanariadha anyakuwa medali ya dhahabu katika mashindano ya mbio ndefu marathon  wanaume  kuwania ubingwa wa riadha duniani yanayoendelea mjini Berlin hapa Ujerumani.

           Kirui alivunja rekodi ya mbio hizo kwa kutumia masaa mawili dakika 6 na sekunde 54 akifuatiwa na mwanariadha mwenzake wa Kenya Emmanuel Mutai aliyeshika nafasi ya pili na kuondoka na medali ya fedha. Mutai alitumia masaa mawili dakika 7 sekunde 48.

        Mwanariadha wa Ethiopia Tsenay Kebede mwenye kushikilia medali ya shaba ya michezo ya Olympiki ameshika nafasi ya tatu baada ya kutumia masaa mawili dakika 8 sekunde 35 na hiyo kujipatia medali ya shaba.

              Huo ulikuwa ni ushindi wa pili wa marathon kwa Kirui mwenye umri wa miaka 27 kufuatia ule wa Vienna hapo mwaka jana. Kirui alikuwa mshindi wa pili katika  michuano ya marathon ya Berlin mwaka 2007 ambapo rekodi ya dunia wakati huo ilikuwa imewekwa na mwanariadha wa Ethiopia Haile Gebrselassie alieshika nafasi ya kwanza.

         Ubingwa wa michuano hiyo ya leo ulikuwa wazi kufauatia  kutoshiriki kwa mwanariadha anayeshikilia rekodi ya dunia Gebrselassie wa Ethiopia,bingwa wa Olympiki wa Kenya Samuel Wanjiru, bingwa wa rekodi ya dunia mara mbili wa Morocco Jaouad Gharib na bingwa mtetezi wa Kenya Luke Kibet .

             Kufikia kilomita 27 mbio hizo zilikuwa zikiongozwa na kundi la wanariadha watatu wa Kenya Mutai,Kirui na Robet Cheruiyot pamoja na Deriba Merga wa Ethiopia  na Dieudonne Disi wa Rwanda. Hata hivyo Disi alishindwa kuendelea na mbio hizo.

       Zikiwa zimebakia kilomita tano Kirui aliweza kumtoka Mutai na kuwa mbele kwa mita 100.

        Mutai mwenye umri wa miaka 24 ambaye ameshinda mbio ndefu za Amsterdam hapo mwaka 2007 alimudu kumaliza mbio hizo licha ya kuonekana hoi wakati akimalizia kilomita ya mwisho.

                 Ushindi wa Kirui unafuatiwa na ule wa ubingwa wa dunia wa Luke Kibet hapo mwaka 2007 na Samuel Wanjiru wa Olympiki hapo mwaka 2008.

              Hivi punde mashindano ya mita 5,000 wanawake yanatazamiwa kuanza na kuna wanariadha wa Kenya wanaoshiriki mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kuwa na msisimko mkubwa kutokana na kuwepo pia kwa wanariadha mahiri wa Ethiopia.

            Miongon wa michuano ya hapo kesho ni fainali za mbio ndefu marathon wanawake fainali za mita 5,000 wanaume mita 1,500 wanawake na mita 800 wanaume.

       Michuano ya ubingwa wa riadha duniani ilioanza mjini Berlin Jumapili iliopita inamalizika hapo kesho.