1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Besigye asema atashinda ingawa haamini uchaguzi utakuwa huru

Mohammed Khelef2 Machi 2016

Siku moja kabla ya upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu nchini Uganda, kiongozi wa upinzani Kizza Besigye anasema ana uhakika wa kushinda ingawa haamini kuwa uchaguzi huo utaendeshwa kwa haki.

https://p.dw.com/p/1Hw5o
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye.
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye.Picha: Reuters/J. Akena

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kampala hivi leo (16 Februari), Besigye alisema mfuasi wake mmoja aliuawa kikatili na polisi hapo jana, wakati walipovamiwa wakiwa kwenye maandamano ya amani.

Zaidi ya 20 kujeruhiwa na wengine kadhaa kukamatwa siku ya Jumatatu wakati waandamanaji walipokabiliana na polisi nchini Uganda kufuatia kukamatwa kwa Besigye.

Besigye, ambaye ndiye mshindani mkuu mbele ya Rais Yoweri Museveni, alikamatwa baada ya kuandamana na maelfu ya wafuasi wake katikati ya mji mkuu, Kampala. Polisi wanasema alichagua kupita njia tafauti na ile aliyopangiwa na jeshi hilo, ambalo nalo lilitumia mabomu ya machozi na risasi za mpira kuwachawanya.

Besigye aliachiliwa muda mfupi baada ya kushikiliwa kwa kile polisi walichosema ni "kwa usalama wake", lakini makabiliano kati ya waandamanaji na polisi yaliendelea hata baada ya hapo, kwa mujibu wa mkuu wa kampeni zake, Wilberforce Kyambadde.

"Mtu mmoja amekufa, lakini bado hatujaweza kuthibitisha sababu ya kifo chake... siwezi kusema idadi ya waliojeruhiwa, lakini tuliwakamata watu 21," alisema naibu msemaji mkuu wa polisi, Patrick Onyango.

Hii ni mara ya pili kwa Besigye kukamatwa kuelekea uchaguzi wa rais wa hapo Alhamis (18 Februari) utakaoshirikisha pia uchaguzi wa wabunge.

Besigye, ambaye alikuwa daktari wa zamani wa Museveni na pia kanali mstaafu wa jeshi, amegombea wadhifa huo wa mara ya tatu dhidi ya Museveni, katika chaguzi ambazo upinzani unasema zilikuwa na wizi wa kura.

Mgombea wa tatu, waziri mkuu wa zamani wa Museveni - Amama Mbabazi, naye pia amewahi kuwekwa ndani kwa muda mfupi.

Makundi ya haki za binaadamu yanamtuhumu Rais Museveni kwa kutumia nguvu kuendeleza utawala wake wa miongo mitatu sasa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa
Mhariri: Saumu Yussuf