1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi mdogo Kenya, wafanyika leo.

Nyanza, Halima11 Juni 2008

Wakenya leo wanapiga kura, kuchagua wabunge wa majimbo matano, ambao unaonekana ni jaribio moja kubwa kwa serikali ya mseto ya nchi hiyo, tangu ilipoanzishwa mwezi April.

https://p.dw.com/p/EHhc
Raia wa Kenya wakiwa wamejipanga mstari kupiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita. ambapo uchaguzi mdogo wa wabunge, unafanyikia leo.Picha: AP

Uchaguzi huo mdogo wa leo nchini Kenya, ni muhimu kwa Rais Mwai Kibaki kutoka chama cha PNU na Waziri Mkuu wake Raila Odinga, kutoka chama cha ODM, kutokana na kwamba kila mmoja anatafuta kuongeza idadi ya wawakilishi wa chama chake, bungeni.

Katika majimbo mawili ya uchaguzi huo wa leo, unalenga kupata wawakilishi wengine wa bunge, kutokana na wale waliochaguliwa awali kuuawa katika matukio mawili tofauti yaliyotokea jijini Nairobi na kaskazini mwa nchi hiyo.

Nafasi nyingine mbili ni kwa ajili ya kujaza nafasi, kutokana na kutotangazwa kwa matokeo ya uchaguzi kufuatia vurugu zilizozuka wakati wa kutangazwa kwa matokeo hayo, kwenye uchaguzi mkuu uliopita na kusababisha matokeo yasitangazwe.

Nafasi nyingine ambayo inajazwa katika zoezi la leo la upigaji kura, ni ile iliyoachwa na Mbunge Kenneth Marende, baada ya kuchuaguliwa kuwa Spika wa bunge la nchi hiyo.

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa mapema huku kukiwa na ulinzi wa polisi, na kwamba hakuna mivutano yoyote iliyoripotiwa, ambapo polisi wamearifu kuwa kumekuwa na amani katika maeneo yote ya nchi, leo asubuhi.

Hata hivyo Uchaguzi huo mdogo unafanyika hii leo, huku baadhi ya watu wakihofia kuibuka tena kwa ghasia za kikabila.

Zaidi ya watu elfu moja na 500 waliuawa, katika mapigano kati ya watu wa makabila yanayohusiana na viongozi wa vyama vya siasa, vilivyokuwa vikipambana vikali katika uchaguzi mkuu uliopita, baada ya kudai kuwa aliyekuwa kiongozi wa upinzani wa nchi hiyo, ambaye sasa ni Waziri Mkuu, Raila Odinga alinyang'anywa ushindi alioupata wa nafasi ya Rais.

Ghasia hizo pia zilisababisha maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao, hususan katika maeneo ya magharibi, ya jimbo la Bonde la Ufa.

Aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Koffi Annan, alifanikiwa kuleta makubaliano ya amani nchini humo, baada ya kuwezesha kuundwa kwa serikali ya mseto, iliyomwezesha Raila Odinga, wa Chama Kikuu cha Upinzani cha ODM, kuwa Waziri Mkuu, na Rais Mwai Kibaki kutoka chama cha PNU kuendelea kushika nafasi yake.

Hata hivyo, mvutano mpya ulionekana tena katika bunge la nchi hiyo, kuhusiana na jinsi ya kuwashughlikia wale wote waliokamatwa kuhusiana na ghasia hizo.

Waziri Mkuu Raila Odinga, alitaka kutolewa msamaha kwa vijana wengi, wakati chama cha PNU kinachoongozwa na Rais Kibaki kilitaka sheria ifuate mkondo wake.

Katika hatua nyingine, uchaguzi huu mdogo wa leo unafanyika huku huzuni ikiwa imetanda, kufuatia ajali ya ndege iliyotokea jana mchana na kusababisha kifo cha Waziri, wa wizara nyeti ya Barabara, Kipkalya Kones pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Lorna Laboso.

Wanasiasa hao ambao wote ni kutoka chama cha ODM, walikumbwa na mauti hayo wakati wakielekea katika eneo la Kichero, Bonde la Ufa, kusaidia wenzao wa ODM, katika kampeni za mwisho za uchaguzi huo wa leo, baada ya ndege hiyo kuanguka katika eneo la Masai Mara.