1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi mkuu Malawi leo

19 Mei 2009

Wapiga kura kumchagua Rais na bunge.

https://p.dw.com/p/HtIR
Rais wa Malawi Bingu wa MutharikaPicha: picture-alliance / dpa

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa tangu saa 12 za asubuhi huku kukiripotiwa milolongo mirefu vituoni katika mji mkuu wa Malawi Lilongwe na ule wa kibiashara wa Blantyre.

Huu ni uchaguzi mkuu wa tatu tangu rais wa zamani na kiongozi wa United Democratic UDF bakili Muluzi alipomaliza utawala wa miaka 30 wa chama kimoja cha Congress cha rais wa kwanza dikteta Hastings Kamuzu Banda 1994.

Wamalawi wapatao milioni 6.5 ikizidi kidogo nusu ya idadi ya wakaazi jumla wa taifa hilo ala kusini mwa Afrika wamejiortodhesha kupiga kura. Kuna wagombea saba katika kinyanaganyiro cha Urais ambacho kinaonekana hasa kuwa ni cha ushindani wa wanasiasa wawili, rais wa asasa Bingu wa Mutharika mwenye umri wa miaka 75 na kiongozi wa upinzani John Tembo mwenye umri wa miaka 77. Rais wa zamani Bakili Muluzi aliyetaka kugombea tena alizuiwa na mahakama

Bakili Muluzi Malawi
Rais wa zamani Bakili Muluzi ambaye mahakama imemkatalia kugombea tena.Picha: picture-alliance / dpa

Bw Mutharika na chama chake cha Democratic Progressive (DPP) wanakabiliwa na changamoto kubwa kutoka kwa Bw Tembo ambaye ni mwanasiasa mkongwe aliyewahi kuwa gavana wa benki kuu na baadae waziri wa fedha wakati wa utawala wa hayati Banda.

Katika kile kinachoonekana kuwa na ushirika wa kushangaza katika siasa za bara la Afrika, chama cha Bw Tembo Malawi Congress kimeingia katika ushirika na chama cha UDF cha Muluzi aliyemn´goa madarakani Dr Banda.

Kuna wagombea 1.100 wanaowania ubunge na idadi ya wanawake safari hii imeongezeka.Wanadadisi wanaashiri kuwa hakuna chama kitakachoweza kupata ushindi wa moja kwa moja na huenda pakahitajika serikali ya mseto.

Umoja wa Ulaya na jumuiya ya madola Commonwealth, zimetuma watazamaji katika ucahaguzi huo, ambao pia unaangaliwa na watazamaji kutoka jumuiya kadhaa barani Afrika. Jumatatu ujumbe wa jumuiya ya madola Commonwealth unaongozwa na rais wa zamani wa Ghana John Koufour uliishutumu televisheni ya taifa, ukisema matangazo yake kuhusiana na uchaguzi huo yanaelemea zaidi upande wa serikali na kuunyima upinzani nafasi sawa.

Rais Mutharika amesema ikiwa atashindwa atajiondoa kabisa katika siasa .

Mwandishi:Mohamed Abdul-Rahman/afpe

Mhariri:Othman Miraji