1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Bavaria na mtihani wa uongozi kwa Merkel

Caro Robi
13 Oktoba 2018

Chama cha Kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU na chama ndugu Christian Social Union CSU vinatazamiwa kukabiliwa na mtihani mkali katika chaguzi za majimbo ya Bavaria na Hesse zinazofanyika mwezi huu.

https://p.dw.com/p/36JID
Wohngipfel im Kanzleramt Merkel und Seehofer
Picha: picture-alliance/dpa/F. Sommer

Übermedien ambayo ni asasi angalizi ya vyombo vya habari imesema kuwa magazeti ya Ujerumani yamekuwa yakichapisha taarifa kuhusu kile kinachotajwa 'mwanzo wa mwisho wa enzi ya Merkel tangu mwaka 2001, mwaka mmoja baada ya kuwa kiongozi wa kwanza mwanamke wa chama cha CDU na miaka minne kabla ya kuchaguliwa kuwa Kansela wa kwanza mwanamke wa Ujerumani.

Licha ya kuwadhihirishia wakosoaji wake uwezo wake wa kuwa kiongozi shupavu kwa miaka 13, katika mkutano wa kila mwaka wa tawi la vijana wa chama cha CDU, ujulikanao kwa kifupi  JU mwishoni mwa wiki iliyopita katika mji wa Kiel, ilikuwa vigumu kutotambua kuwa pole pole kwa kweli enzi ya utawala wa Merkel iko karibu kufikia ukingoni.

Mwezi uliopita, Merkel alimpoteza mmoja wa washirika wake wa karibu bungeni baada ya wabunge wa vyama vya kihafidhina CDU/CSU kumuondoa madarakani Volker Kauder kuwa kiongozi wao bungeni.

Kitendo cha kuondolewa kwa Kauder ambaye amekuwa kiongozi wa CDU/CSU bungeni tangu 2005 na nafasi yake kuchukuliwa na Ralph Brinkhaus, kulionekena thibitisho kuwa Merkel anapoteza uungwaji mkono miongoni mwa hata wabunge wa chama chake.

Deutschland CSU Parteitag in München | Markus Söder
Waziri mkuu wa Bavaria Markus Soeder na mgombea mkuu wa chama cha CSU katika uchaguzi wa Oktoba 14.Picha: Getty Images/S. Gallup

Wabavaria wasiopendezwa

Hilo lilikuwa bayana wakati kiongozi JU Paul Ziemiak ailiposhangiliwa sana kwa kumtaka Merkel kukifanyia mageuzi chama chake ili kiendane na wakati na kulikuwa na manung'uniko kutoka kwa wajumbe wa Bavaria ambao wako katika mkondo wa mwisho wa kampeini kabla ya uchaguzi wa jimbo hilo unaofanyika Jumapili hii.

Pia ni wazi kuwa Merkel kwa kiasi kikubwa ameachjwa nje ya kampeini za vyama hivyo vya kihafidhina huku kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miongo mingi, CSU kina uungwaji mkono mdogo mno miongoni mwa wapiga kura wa Bavaria.

Wakati wajumbe wa chama chake cha CDU wakisimama kumshangilia alipowasili katika mkutano huo wa JU, wajumbe wa CSU walisalia kuketi katika viti vyao alipoingia ukumbini na wengine walionekana kujishughulisha zaidi na simu zao na kusoma magazeti katika kipindi cha nusu saa za hotuba ya Merkel.

Mmoja wa wajumbe wa Bavaria Matthias Büttger alikuwa hata na uthubutu wa kusimama na kumueleza Merkel kuwa hawaamini tena kuwa vyama vya Kihafidhina vinaweza kupiga hatua mbele akiendelea kuwa kiongozi wao.

Mabadiliko kutokea juu?

Mjumbe mwingine wa CSU Thomas Haslinger ameiambia DW Kuwa kutoridhika na uongozi wa Merkel bado kumejikita katika sera yake kuhusu uhamiaji baada ya kuwaruhusu maelfu ya wakimbizi na wahamiaji mwaka 2015 kuingia Ujerumani.

CSU-Parteitag und Wahlkampfkundgebung
Mwenyekiti wa CSU na waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer.Picha: picture alliance/AP/M. Schrader

Haslinger amesema kabla ya hapo, chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Altenrative für Deutschland AfD kilikuwa hakina nguvu wala ushawishi wa maana.

Lakini tangu Merkel kufungua mipaka ya Ujerumani kuwaruhusu zaidi ya wahamiaji milioni moja kuingia nchini humo, wapiga kura walikerwa na hivyo kukigeukia chama kinachowapinga wahamiaji cha AfD na hivyo kukipa nguvu na kukifanya chama chenye ushawishi mkubwa mashariki mwa Ujerumani hivi sasa.

Lakini licha ya manunguniko kutoka kwa Wabavaria, Merkel anasalia kuwa maarufu katika chama chake cha CDU.

Kwa hivyo hata kama chaguzi za majimbo ya Bavaria na Hesse zitakwenda vibaya kwa CSU na CDU, ni wachambuzi wachache wa kisiasa wanaoamini kuwa atapata mshindani mwenye nguvu katika mkutano wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika mjini  Hamburg mwezi Desemba kumchagua kiongozi mpya wa CDU.

Mwandishi: Caro Robi/DW

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman