1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Bunge la Ulaya waendelea

Mohammed Khelef
26 Mei 2019

Wapigakura katika mataifa zaidi ya 20 ya Umoja wa Ulaya wanapiga kura zao muda huu kuchaguwa wawakilishi watakaoziwakilisha nchi zao kwenye Bunge la Ulaya huku kukiwa na wasiwasi dhidi ya siasa kali za mrengo wa kulia.

https://p.dw.com/p/3J5wZ
Berlin - Frank-Walter Steinmeier und seine Frau Elke Buedenbender bei Stimmabgabe zur Europawahl
Picha: Reuters/F. Bensch

Raia nchini Ufaransa na Ujerumani wanapiga kura leo katika siku ya mwisho ya uchaguzi wa Bunge la Ulaya ambapo vyama vinavyopinga Umoja wa Ulaya pamoja na uhamiaji vinatumai kutoa changamoto kubwa.

Mbali ya Ujerumani na Ufaransa, ambayo ni mataifa yenye nguvu barani Ulaya, nchi nyingine karibu 20 wanachama wa Umoja huo zinapiga kura leo, ambayo ni siku ya mwisho ya uchaguzi huo wa Bunge la Ulaya.

Zaidi ya wapiga kura milioni 400 wanashiriki uchaguzi huo katika mataifa 28 na matokeo rasmi yanatarajiwa baadaye leo jioni.

Nchini Ujerumani, maoni ya umma ya kabla ya uchaguzi yalivipa nafasi ya ushindi wa asilimia 28 vyama ndugu vya kihafidhina vya CDU na CSU.

Wanasiasa kutoka vyama vikuu nchini Ujerumani walitumia siku za mwisho kabla ya uchaguzi kutoa onyo dhidi ya kukipigia kura chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, AfD, kinachopinga wahamiaji na Umoja wa Ualya.