1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Irak. Usalama waimarishwa.

Eric Kalume Ponda30 Januari 2009

Raia wa Irak wanajiandaa kwa uchaguzi wa mabaraza ya majimbo uchaguzi ambao ni wakwanza tangu mwaka wa 2005 huku hali ya usalama ikiimarishwa.

https://p.dw.com/p/GkAf
Raia wa Irak katika kampeni za hivi punde. Mbivu na mbichi ni hapo kesho.Picha: AP


Hali hiyo inafuatia mauaji ya wagombea sita ambao wameuawa tangu kampeni za uchaguzi zianze.Tayari kampeni zimemalizika mapema leo asubuhi huku uchaguzi huo ukitajwa kuwa sawa na kura ya maoni kwa utawala wa waziri mkuu Nuri al-Maliki.


Hali ya wasi wasi inazidi kutanda nchini Irak kabla ya uchaguzi wa hapo kesho, kufuatia mauaji ya jana ya wagombea watatu na wanaharakati wao wa kisiasa katika miji wa Baquba na Mosul kaskazini mwa mji mkuu Baghdad.


Mauaji hayo yanayodaiwa kutekelezwa na makundi ya wapiganaji, yanahofiwa huenda sehemu ya njama ya kutaka kuvuruga shughuli hiyo ya uchaguzi.


Wafuasi wa makundi ya wapiganaji jana walifyatulia risasi na kumuua mgombea wa chama cha Irak Concord Front Omar Faruq al-Ani, ambaye chama chake ndicho kikbwau miongoni mwa vile vya Wasunni bungeni.


Mgombea wa pili kuuawa ni Hazim Salim Ahmed pia Msuni ambaye amekuwa akipigania umoja wa taifa nchini humo, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi nje ya nyumba yake mjini Mosul, mji unaoaminika kuwa ngome ya mwisho ya wafuasi wa kundi la kigaidi la Al- Qaeda nchini Irak.


Serikali ya Irak imefunga mipaka yake kama sehmu ya kudumisha usalama kutokana na hofu ya mashambulio zaidi kutoka kwa makundi yaliyoko nje ya nchi hiyo yanayoipinga serikali ya waziri mkuu Al Maliki.


Maafisa watatu wa kikosi cha polisi cha kutegua mabomu pia wameuawa hivi leo, baada ya bomu la kutegwa ardhini kulipuka katika kambi yao mjini Diwaniyah. Bomu hilo lilipatikana limetegwa kando ya barabara, na kulipuka katika kambi hiyo wakati maafisa hao walipokuwa wakijaribu kulitegua.

Eneo la Diwaniyah limekumbwa na mapigano makali baina ya kambi mbili za Washia, lile linalomuunga mkono kiongozi wa kidini Moqtada al-Sadr, anayepingwa vikali na Marekani na lile linalounga mkono baraza kuu la Waislamu la Iraq, ambalo ni mwanachama wa serikali ya muungano bungeni.

Uchaguzi huu pia unaochukuliwa sawa na kura ya maoni kwa utawala wa waziri mkuu Nuri Al Maliki, ni wa kwanza kufanyika bila ya kusimamiwa na wanajeshi wa Marekani ambao wamekuwa wakidumisha usalama nchini humo tangu Marekani ilipoivamia nchi hiyo.


Uchaguzi huo unafanyika katika majimbo 14 kati ya 18, na unachukuliwa kwaumuhimu mkubwa kama mtihani wa uidhabiti wa taifa hilo tangu kuanguka kwa utawala wa rais wa zamani Saddam Hussein.


Hata hivyo uchaguzi huo hautafanyika katika majimbo 4 katika majimbo ya Wakurdi, ikiwa ni jimbo la Arbi, Dohuk na Sulaimaniyah. Kadhalika uchaguzi huo pia umeahirishwa katika jimbo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Kirkuk ambalo Wakurdi wanataka lijumuishwe kwenye mamlaka yao, licha ya upinzani mkali kutoka kwa serikali kuu mjini Baghdad.


Uchaguzi uliofanyika mwaka wa 2005 ulisusiwa na Wasuni wengi lakini wadadisi wansema kuwa huenda wakajitokeza kupambana na Washia walio wengi nchini Iraq.