1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi wa China wastawi tena

Abdu Said Mtullya18 Oktoba 2013

Pato jumla la ndani la China limestawi kwa asilimia 7.8 kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa leo, baada ya ustawi wake wa uchumi kulega lega katika robo mbili za mwaka

https://p.dw.com/p/1A2Kq
Uchumi wa China wastawi tena
Uhumi wa China wastawi tenaPicha: picture-alliance/dpa

Licha ya ustawi huo wachambuzi wana wasi wasi iwapo kuboreshwa kwa hali ya ndani kutaweza kuendelezwa katika nchi hiyo ambayo ni injini muhimu ya ustawi wa uchumi wa dunia.

Matokeo hayo ya pato jumla la taifa yamelingana na utabiri katika uchunguzi uliofanywa na wachambuzi 11 wa shirika la AFP. Kwa mujibu wa idara ya taifa ya takwimu,ustawi katika kipindi cha miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu ulifikia asilimia 7.7.

Uchumi wote kwa jumla ulistawi kwa uthabiti na ulikuwa na kasi nzuri.

Ishara zote zilibakia katika eneo imara na hivyo kuweza kuchangia katika kuleta mageuzi ya muundo na kusonga mbele na mageuzi. Hata hivyo msemaji wa idara ya takwimu ya China ametahadharisha juu ya mashinikizo ambayo ni hali tata za ugeugeu kutoka nje,na pia ametahadharisha juu ya matatizo ya kiuchumi yanatokana na miundo sugu ya muda mrefu. Msemaji huyo pia ameeleza kwamba takwimu linganifu juu ya miezi mitatu iliyopita zinaweza kuwa na maana kwamba ustawi hausongi mbele hadi katika robo ya nne ya mwaka.

Takwimu zilizopo zinaashiria kwamba China imo katika mkondo sahihi kwa maana ya kuweza kuyafikia malengo yake ya mwaka huu ya ustawi wa asilimia 7.5 Hata hivyo serikali ya China hutangaza takwimu za makisio ambazo baadae huvukwa na takwimu halisi.

Uzalishaji viwandani ambao ni kipimo cha tija viwandani uliongezeka kwa asilimia 10.2 katika mwezi uliopita sawa na mwaka uliotangulia.Kwa mujibu wa idara ya takwimu mauzo ya reja reja ambayo ni kipimo cha utashi wa ndani yaliongezeka kwa asilimia 13.3. Na uekezaji katika mali za kudumu ambao ni kipimo cha matumizi ya serikali katika sekta ya miundombinu uliongzeka kwa asilimia 20.2 katika kipindi cha miezi tisa ya kwanza.

Taarifa za uchumi wa China zimetolewa wakati ambapo utawala mpya wa nchi hiyo unasisitiza haja ya kubadilisha misingi ya ustawi na kulekea katika ruwaza ambapo utashi unadumishwa .Wataalamu waliohojiwa kabla ya kutolewa kwa taarifa walisema kwamba ustawi umetokana hasa na mpango wa serikali wa kuuchochea uchumi wa tokea mwezi wa juni mwaka jana.

Mwandishi;Mtullya Abdu.afp

Mhariri:Yusuf Saumu