1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi wa dunia wadorora

Hamidou, Oumilkher13 Novemba 2008

Makadirio ya kiuchumi kwa mwaka huu wa 2008 na mwaka 2009 si ya kutia moyo

https://p.dw.com/p/Ftsc
Soko la hisa la mjini FrankfurtPicha: AP


Jumuia ya ushirikiano na maendeleo ya kiuchumi-OECD,imerekebisha hii leo makadirio ya ukuaji wa kiuchumi kwa Marekani,Japan na nchi zinazotumia sarafu ya Yuro kutokana na ile hali kwamba shughuli za kiuchumi katika eneo lote hilo linalojumuisha nchi 30,zinadorora.


Jumuia ya OECD inakadiria upungufu wa asili mia mbili nukta 8  katika pato la ndani la Marekani,mnamo robo ya nne ya mwaka huu-hali itakayopelekea ukuaji wa kiuchumi wa dola hilo kubwa kabisa la kiuchumi ulimwenguni kufikia asili mmia 1.4 kwa mwaka huu wa 2008.Kwa mwaka 2009,ukuaji wa kiuchumi wa Marekani utapungua na kusalia asili mia sifuri nukta tisaa.


Nchi za zoni ya Yuro na Japan nazo pia zitateleza na shughuli zao kuzorota.


Pato la ndani la Japan litapungua kwa asili mia sifuri nukta moja mnamo robo ya mwisho ya mwaka huu,sawa na hali namna itakavyokua mwaka mzima wa 2009.Na katika zoni ya Yuro pato hilo la ndani litapungua kwa asili mia moja kwa robo ya mwisho ya mwaka huu na asili mia sifuri nukta tano mwakani.


"Makadirio ya OECD yanaashiria uwezekano wa kuendelea kuzorota shughuli za kiuchumi" imetajwa katika taarifa ya jumuia hiyo yenye makao yake makuu mjini Paris nchini Ufaransa.


Ripoti hiyo imechapishwa muda mfupi kabla ya mkutano wa mjini Washington utakaowaleta pamoja viongozi wa mataifa 20 kuzungumzia mzozo wa fedha ulimwenguni.


Taarifa hiyo imetangazwa pia mnamo wakati ambapo wataalam wa tano wa kiuchumi wa Ujerumani wamewasilisha ripoti yao inayoashiria pia kuzorota shughuli za kiuchumi nchini Ujerumani.


Kufumba na kufumbua faharasa katika masoko takriban  ya hisa zikaanza kuporomoka baada ya dola hili kuu la kiuchumi barani Ulaya, kutamka rasmi  shughuli zake za kiuchumi zimeanza kupooza.


Nchini Uengereza pia,zahma ya mzozo wa fedha imeanza kuyatikisa makampuni kadhaa na kuhatarisha nafasi za kazi.Kampuni kubwa la mawasiliano ya simu BT limetangaza azma ya kufutilia mbali nafasi elfu kumi za kazi,ikiwa ni sawa na asili mia sita ya wafanyakazi wake wote,katika wakati ambapo shughuli za kiuchumi za nchi hiyo zinaanza kudorora.



Wawekezaji wa Ujerumani wameduwaa kufuatia habari za kutuwama shughuli za kiuchumi ,kwa mara ya kwanza tangu miaka mitano iliyopita.Chanzo cha hali hiyo ni mzozo wa fedha unaoikaba dunia wakati huu tulio nao.


Farahasa katika soko la hisa la mjini Frankfurt zilianguka kwa asili mia sifuri nukta 49 leo mchana kabla ya kupanda baadae.Soko la hisa la mjini London,limemalizika kwa kasoro .


Licha ya kishindo cha kuzorota shughuli za kiuchumi nchini Marekani,Japan na katika nchi za zoni ya Yuro,wataalam wa kiuchumi wa jumuia ya ushirikiano na maendeleo ya kiuchumi OECD hawaamini kama hali hiyo itaselelea.


OECD inaashiria ukuaji wa kiuchumi wa asili mia 1.6 kwa Marekani,asili mia moja nukta mbili kwa zoni ya Yuro na asili mia sifuri nukta sita kwa Japan ifikapo mwaka 2010.