1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya leo ya Ujerumani

Josephat Charo4 Oktoba 2006

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wamejihusisha na maadhimisho ya miaka 16 ya muungano wa Ujerumani na mkutano wa leo wa chama cha SPD na chama cha CDU- CSU kuhusu mabadiliko ya mfumo wa afya.

https://p.dw.com/p/CHUm

Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel aliwahimiza wajerumani wajiandae kwa mabadiliko makubwa. Akizungumza mjini Kiel wakati wa maadhimisho ya miaka 16 ya muungano wa Ujerumani Bi Merkel amesema watu wasiulize mambo yasiyokwenda sawa bali waulize ni mambo gani yanayoendelea. Huu ndio uliokuwa msimamo wake kuhusu muungano kama mjerumani kutoka eneo la mashariki.

Mhariri wa gazeti la Stuttgarter Nachrichten anasema Ujerumani imembadili Bi Merkel, lakini pia Ujerumani yenyewe imebadilika. Na kuna sababu nyingi za kujivunia mabadiliko mbalimbali katika jamii, uchumi na siasa tangu siku za muungano.

Wajerumani wanawakilishwa na muungano unaokabiliwa na changamoto kubwa. Kubadilika kwa sera kunaonekana na wengi kuwa mbali kama ilivyokuwa hapo awali. Kansela Merkel bado anajua vipi swala hili lisivyoridhisha.

Gazeti la Ostsee Zeitung la mjini Rostock kuhusu mada hii limesema kansela Merkel anayetokea mashariki mwa Ujerumani amejaribu katika hotuba yake ya kibinafsi kutoa himizo. Kwa uwazi ameeleza umuhimu wa muungano halisi kuliko fedha zinazotolewa na serikali na majimbo ya magahribi kulijenga eneo la mashariki na miradi ya mabadiliko isiyo na faida, ambayo ni nadra kuwekwa wazi kwa raia.

Ujerumani inahitaji mashikamano na lengo la pamoja litakaloweza kuibeba mizigo na matatizo yaliyopo na hatimaye kuyatatua.

Mhariri wa gazeti la Handelsblatt anasema maadhimisho yana athari mbaya zinazokaribisha matamshi ya kijumla yasiyozingatia hali halisi na yasiyokuwa na maana. Kama vile Ujerumani Mashariki imefika wapi miaka 16 tangu muungano? Swali hili linalopendwa na wengi halina maana tena kwa kuwa mtazamo wa eneo la mashariki huzungumziwa tu wanaotoa hotuba. Lakini ukweli ni kwamba mengi yamebadilika.

Gazeti la Mitteldeutsche linasema kimsingi kuna tatizo moja. Majimbo mapya ya Ujerumani mpaka leo yanaweza kulipa gharama kati ya asilimia 40 na 50 kutumia kodi zao. Fedha nyengine hutoka kwa serikali na majimbo ya magharibi. Kuanzia mwaka wa 2009 mpango huu utaondolewa na jimbo ambalo halitakuwa limeweka sawa bajeti yake, litakuwa na nafasi ndogo katika kila hali.

Mada ya pili inahusu mkutano wa leo kuhusu mivutano ya mabadiliko ya mfumo wa afya hapa Ujerumani. Gazeti la FrankfurterAllgemeine limesema mkutano huo hauhusu makubaliano kati ya chama cha CDU na pendekezo lake la kiwango kitakachotozwa, na chama cha SPD kinachosisitiza bima ya raia.

Makubaliano haya hayatafikiwa. Viongozi wa vyama wanatakiwa kuweka wazi pendekezo lao kwa wanasiasa wanaohusika na maswala ya afya waweze kulielewa, ambao wamelielewa kuwa lisilo na ufanisi wowote.

Kuhusu mkutano huo mhariri wa gazeti la Volksstimme amesema hapana hakutakuwa na ufanisi mkubwa. Mzozo wa mabadiliko ya mfumo wa afya umedhihirisha udhaifu wa serikali ya muungano mjini Berlin.