1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UEFA yaanzisha mashindano mapya ya soka Ulaya

Sylvia Mwehozi
12 Septemba 2018

Raundi ya pili ya mechi za mashindano mapya ya ligi ya Mataifa ya Ulaya imekamilika siku ya Jumanne, baada ya Uhispania kuibugiza Croatia mabao 6-0.

https://p.dw.com/p/34lfl
Fußball Nations League München Deutschland vs Frankreich
Picha: Getty Images/AFP/F. Fife

Mashabiki wengi bado wanajitahidi kuelewa wazo la ligi hiyo ya mataifa wakati ikiendelea, huku pia wachezaji wenyewe bado hawajapata uelewa wa kutosha, ambapo mlinzi wa England Harry Maguire alikiri wiki iliyopita kwamba "inachanganya, lakini tunajaribu kuelekeza vichwa vyetu mbele". Lakini wakati mchakato unaoruhusu kufuzu michuano ya Ulaya ya 2020 ukiwa hauko wazi, wazo la msingi la kupanda na kushuka kwa timu ni rahisi kulielewa.

Matokeo yalivyokuwa

Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps alikibakisha kikosi chake kilichoshinda kombe la dunia mwezi Julai. Ufaransa ilitoka sare ya bila kufangana na Ujerumani na kushinda nyumbani mabao 2-1 dhidi ya Uholanzi. Ufaransa imedhamiria kushinda ufunguzi wa mashindano ya kombe la ligi ya Mataifa, ambapo jumla ya timu nne zitakazofuzu fainali zitachuana mwakani mwezi Juni.

Hispania ilipata matokeo ya kushangaza baada ya kuwachapa Croatia mabao 6-0 na haikuwa rahisi kufikiria matokeo waliyoyapata dhidi ya Urusi wakati wa kombe la dunia baada ya kutolewa kwa mikwaju ya penalti. Kichapo walichokitandaza dhidi ya washindi nambari mbili wa dunia, siku tatu baada ya kuwashinda England katika uwanja wa Wembely, kilikuwa ni ukumbusho kwamba Hispania bado ni timu iliyosheheni wachezaji mahiri katika dunia.

Fußball Nations League -  Italien- Polen
Ligi A kundi la tatu, mechi kati ya Hispania na PolandPicha: Reuters/S. Rellandini

Italia ilitoka sare na Poland na kupoteza dhidi ya Ureno. Kocha wa Italia, Roberto Mancini, anajaribu kukifufua kikosi cha Azzuri baada ya kikosi hicho kushindwa kufuzu kombe la dunia la mwaka huu, lakini inaonekana mgogoro unazidi kuwa mkubwa. Je, Italia itakuwa timu itakayoshuka kutoka juu kutoka ligi ya mataifa? Mancini anasema "tusubiri na tuone, lakini lengo letu ni kutengeneza kikosi cha michuano ya Ulaya ya 2020'.

Kuongezwa kwa timu na kufikia 24 kumeshuhudia nchi tano zikiingia katika michuano ya Ulaya mwaka 2016 na kuanza kwa ligi ya Mataifa kunawezekana kukafungua milango kwa nchi nyingine katika toleo la 2020. Finland iko katika Ligi C na Ligi D ikiwa na Georgia, Luxembourg, na Macedonia zilijinyakulia pointi za juu kutoka michezo miwili ya ufunguzi na kuweka matumaini ya kufikia hatua ya mtoano itakayoamua fainali kwa wale watakaofuzu. Kosovo pia inaongoza kundi lake baada ya kupata ushindi dhidi ya Faroe Islands wa mabao 2-0.

Ligi ya Mataifa ya Ulaya ni mashindano mapya ambayo yanaandaliwa na shirikisho la soka barani Ulaya UEFA, ambayo imegawanya timu za taifa kwenye ligi nne ambazo zina makundi manne. Timu ya kwanza inajumuisha timu bora kwa mujibu wa jedwali la FIFA kufikia mwezi Oktoba mwaka jana.

Hadi kufikia mwakani, timu bora kutoka kila kundi na kila ligi zitapandishwa kucheza ligi ya juu inayofuata, huku timu za mwisho zikishushwa ligi ya chini. Kila timu bora katika kila ligi itafuzu nusu fainali ya ligi hiyo na fainali itafanyika mwezi Juni mwakani.

Mwandisi: Sylvia Mwehozi/afpe

Mhariri: Josephat Charo