1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yafanya mashambulizi ya anga Syria

27 Septemba 2015

Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema nchi yake imefanya mashambulizi yake ya kwanza ya anga Jumapili (27.09.2015) dhidi ya makambi ya mafunzo ya kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1GeKy
Ndege ya kivita ya Ufaransa.
Ndege ya kivita ya Ufaransa.Picha: picture-alliance/AP Photo/Bob Edme

Hollande amekaririwa akisema muda mfupi baada ya Ufaransa kuamuru mashambulizi hayo " vikosi vyetu vimeshambulia maeneo yaliyokusudiwa. " karibu na mji wa Deir Ezzor.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa amesema Ufaransa imeishambulia kambi ya mafunzo ya kundi la kigaidi la Daesh ambalo linatishia usalama wa nchi yao na kuongeza kwamba mashambulizi zaidi yanaweza kuamuriwa wiki zinazokuja.

Hollande ambaye amekuwa kwenye shinikizo la kisiasa kuchukuwa hatua dhidi ya kundi hilo la Dola la Kiislamu kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi nchini Ufaransa amesema Ufaransa inazungumza na kila mtu na hakuna inayemtenga.

Mashambulizi hayo yanatimiza ahadi ya Ufaransa ya kupambana na kundi hilo ambalo rais huyo wa Ufaransa amesema linapanga mashambulizi dhidi ya nchi kadhaa ikiwemo Ufaransa.

Mashambulizi yazingatia ujasusi

Taarifa ya ofisi ya rais imesema Ufaransa imefanya mashambulizi nchini Syria kwa kuzingatia taarifa za ndege za upelelezi uliofanyika nchini humo mapema mwezi huu.Taarifa hiyo haikutowa ufafanuzi zaidi.Taarifa hiyo imesema " taifa letu litashambulia kila pale usalama wetu wa taifa utakapokuwa hatarini."

Rais Francois Hollande wa Ufaransa.
Rais Francois Hollande wa Ufaransa.Picha: Reuters/C. Platiau

Wizara ya ulinzi ya Ufaransa imesema mapema mwezi huu kwamba Ufaransa imefanya mashambulizi ya anga 215 dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali wa kundi hilo la Dola la Kiislamu nchini Iraq ikiwa sehemu ya mashambuzi ya majeshi ya muungano unaongozwa na Marekani tokea mwaka jana

Awali Ufaransa ilikuwa ikisita kufanya mashambulizi hayo nchini Syria kutokana na wasi wasi wa kumnufaisha Rais Bashar Assad na haja kwa hatua hiyo kuchukuliwa kwa kuzingatia sheria ya kimataifa.

Kubadili mkakati

Kufuatia kubadilika kwa mkakati huo kulikotangazwa na Hollande mapema mwezi huu ofisi hiyo ya Rais Hollande imetaja hapo Jumapili "uhalali wa kujihami " uliotamkwa na katiba ya Umoja wa Mataifa kuunga mkono mashambulizi hayo ya kijeshi.

Rais Bashar Assad wa Syria akizungumza na wanajeshi wake walioko kwenye mapambano
Rais Bashar Assad wa Syria akizungumza na wanajeshi wake walioko kwenye mapambanoPicha: picture-alliance/AP Photo

Hollande ambaye huko nyuma alifuta uwezekano wa kutuma wanajeshi wa ardhini nchini Syria ametaja ushahidi unaothibitisha mipango ya kuishambulia Ufaransa na kuongezeka kwa hatari dhidi ya raia wa Syria jambo lililopelekea maelfu kwa maelfu kuikimbia nchi hiyo.

Ofisi hiyo ya rais imesisitiza hoja ya Ufaransa kwamba mashambulizi hayo ya anga nchini Syria ni suala la kulihami taifa.Ufaransa tayari imeshambuliwa na watu wa itikadi kali wanaodai kuwa na mafungamano na kundi la Al Qaeda.

Wakati hakuna ufafanuzi uliotolewa juu ya mahala kukikofanyika mashambulizi hayo au wakati mashambulizi hayo yalipofanyika Waziri Mkuu wa Ufaransa Manuel Valls amesema Ufaransa inayaandama maficho ya kundi hilo la Dola la Kiislamu ambapo wale wanotaka kuishambulia Ufaransa wanapatiwa mafunzo.

Juhudi za Ufaransa

Generali Vincent Desportes amekiambia kituo cha televisheni cha iTele TV kwamba lengo ni kulishambulia kundi hilo la Dola la Kiislamu hatua kwa hatua,kulivunja na ikiwezekana kuwazuwiya wanamgambo wake kujipenyeza nchini Ufaransa.

Wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu.
Wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu.Picha: picture-alliance/AP Photo

Ufaransa imeendelea kupinga mapendekezo ya kidiplomasia ya hivi karibuni ya kumuachia Rais Bashar Assad wa Syria kuedelea kubakia madarakani kwa kipindi fulani.

Serikali ya Ufaransa imesisitiza kwamba wakati ikiwa sehemu ya muungano unaongozwa na Marekani hujiamulia yenyewe nani na kipi cha kushambulia.

Hollande alitangaza hapo Septemba saba nia ya Ufaransa kuanza mashambulizi ya anga nchini Syria baada ya kuibuka kwa picha ya mvulana wa umri wa miaka mitatu wa Syria akiwa amekufa ufukweni jambo lililoufadhaisha umma wa dunia juu ya wakimbizi wa Syria wanaokimbia kunusuru maiasha yao.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP/AP

Mhariri : Yusra Buwayhid