1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugaidi waua 84 Nice Ufaransa

John Juma15 Julai 2016

Mshambuliaji alilivurumisha lori katika eneo lenye mkusanyiko wa watu waliokuwa wakifurahia maonyesho ya fataki katika sherehe ya siku ya kitaifa. Zaidi ya watu 80 wakiwemo watoto walifariki kwa kugongwa na Lori hilo.

https://p.dw.com/p/1JPNL
Eneo la shambulio Nice.
Eneo la shambulio Nice.Picha: Reuters/E. Gaillard

Watu wasiopungua 84 wameuawa katika shambulio ambalo limetajwa kuwa la kigaidi katika mji wa Nice kusini mwa Ufaransa. Hii ni baada ya mshambuliaji alietambuliwa kuwa mwenye uraia wa Ufaransa na Tunisia kuliendesha lori kwa mwendo kasi katika umati wa watu waliokuwa wamekusanyika kusherehekea siku kuu ya taifa la Ufaransa.

Inaarifiwa kuwa jamaa aliyejihami kwa bunduki aliliendesha lori ndani ya mkusanyiko wa watu waliokuwa wakifurahia maonyesho ya fataki, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 80. Watu hao walikusanyika kusherehekea siku ya kitaifa ya Ufaransa ijulikanayo kama Bastile. Polisi walimpiga risasi na kumuua dereva wa lori hilo baada ya kuendesha lori hilo takriban kilomita mbili ndani ya eneo lililokuwa na umati huo wa watu.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande ametaja shambulio hilo kuwa la kigaidi, na Ufaransa imetangaza siku tatu za maombolezo kwa waliofiwa kwanzia kesho. Hollande anasema: "Hakuna kukataa hili ni shambulizi la kigaidi, kwa mara nyingine aina mbaya sana ya shambulio. na ni wazi kuwa tunapaswa kufanya kila jambo kutuwezesha kupigana dhidi ya janga la ugaidi."

Nimeamua kwamba sheria ya hali ya hatari iliyopaswa kuisha tarehe 26 mwezi huu sasa itaongezwa kwa miezi mitatu zaidi. Mswada utawasilishwa bungeni wiki ijayo. hakuna kitakachotuzuia kupigana na ugaidi. na kwa mara nyingine tutaimarisha juhudi zetu Syria na Iraq na tutazidi kushambulia wale wanaotulenga katika ardhi yetu.

Jamaa aweka shada la maua kuomboleza.
Jamaa aweka shada la maua.Picha: picture-alliance/dpa/Tass/S. Savostyanov

Jamaa mmoja kwa jina Nader aliyeshuhudia kisa chote aliambia runinga ya BFM kwamba awali alifikiria dereva wa lori hilo alikosa mwelekeo. Baada ya kugonga na kukanyaga watu kadhaa wakiwemo watoto, alichukua bunduki yake na kuanza kufyatulia polisi, kabla ya polisi kumuua. Duru karibu na upelelezi umesema gruneti isiyofanya kazi pamoja na bunduki bandia nazo zilipatikana kwenye lori hilo. Hollande anasema:

"Nimeamua kwamba sheria ya hali ya hatari iliyopaswa kuisha tarehe 26 mwezi huu sasa itaongezwa kwa miezi mitatu zaidi. Mswada utawasilishwa bungeni wiki ijayo. hakuna kitakachotuzuia kupigana na ugaidi. na kwa mara nyingine tutaimarisha juhudi zetu Syria na Iraq na tutazidi kushambulia wale wanaotulenga katika ardhi yetu."

Mshambuliaji atambuliwa

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31 ametambuliwa kuwa raia wa Ufaransa mwenye asili ya Tunisia. Hata hivyo hakuwa katika orodha ya washukiwa wa ugaidi japo amehusishwa na visa vya uhalifu mathalan wizi wa kimabavu na kuzua vurugu.

Wahudumu zaidi wa afya wametumwa katika mji wa Nice ili kusaidia katika kutambua miili haraka kusudi iwasilishwe kwa familia zao mapema.

Shambulizi hilo ni la tatu dhidi ya Ufaransa katika muda wa miezi kumi na minane iliyopita. Ni shambulizi linalojiri miezi minane baada ya Dola la kiislamu kushambulia maeneo ya burudani mjini Paris na kuu watu 130.

Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga