1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ugiriki laidhinisha mapendekezo mapya ya kiuchumi

11 Julai 2015

Wakopeshaji wa kimataifa wameridhika na mapendekezo mapya yaliyowasilishwa na serikali ya Ugiriki juu ya mageuzi na Bunge la nchi hiyo pia limeyapitisha mapendekezo hayo.

https://p.dw.com/p/1Fx3h
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis TsiprasPicha: Reuters

Duru za Umoja wa Ulaya zimeyasema hayo kwa shirika la habari la Ujerumani dpa.Duru hizo zimesema mapendekezo hayo mapya yanafaa sana kuwa msingi wa kutolewa fedha nyingine, kiasi cha Euro Bilioni 74 ,kwa ajili ya kuinusuru Ugiriki.

Afisa wa Umoja wa Ulaya ambaye hakutaka kutajwa, aliyeitoa taarifa hiyo,ameeleza kuwa mpango mpya wa Ugiriki umetathminiwa kuwa unafaa, na kwa hivyo mfuko wa uokozi wa Umoja wa Ulaya, ESM upo tayari kutafakari kutenga kiasi cha Euro Bilioni 58 pamoja na kiasi cha Euro Bilioni 16 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa IMF.

Fedha hizo zitakuwa fungu la tatu katika mpango wa kuiokoa Ugiriki.Tathmini iliyofanywa na wakopeshaji wa Ugiriki ya mpango wa mageuzi wa nchi hiyo, sasa itawasilishwa kwa mawaziri wa fedha wa nchi 19 za ukanda wa sarafu ya Euro wanaokutana leo Jumamosi.

Bunge la Ugirki
Bunge la UgirkiPicha: Reuters

Hata hivyo uwezekano wa mpango huo kupitishwa ni nusu kwa nusu, kutokana na upinzani wa nchi zenye msimamo mkali kama vile Ujerumani inayopinga wazo la kuifutia Ugiriki deni lake.

Mawaziri hao wa fedha wataiandaa ripoti kwa ajili ya viongozi wa ukanda wa sarafu ya Euro watakaokutana hapo kesho, na kufuatiwa na kikao cha dharura cha viongozi wa nchi 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Bunge layapitisha mageuzi

Bunge la Ugiriki limeyaridhia mapendekezo ya serikali juu ya mpango mpya wa mageuzi ambao Waziri Mkuu Alexis Tsipras amewaahidi viongozi wenzake wa Umoja wa Ulaya ,ili nchi yake ipewe fedha nyingine na hivyo kuiepusha kujiondoa kwenye sarafu ya Euro. Kwa mujibu wa taarifa ya Televisheni ya serikali wabunge zaidi ya 251 wameuunga mkono mpango wa serikali.

Katika mapendekezo mapya yaliyotolewa na Ugiriki ili ipatiwe mkopo wa miaka mitatu, Waziri Mkuu Tsipras ameyazingatia mambo muhimu ikiwa pamoja na matakwa ya wakopeshaji wa kimataifa juu ya kuleta mageuzi katika mfumo wa pensheni, kupandisha kodi ya mauzo na kukubali kuutekeleza mpango wa ubinafsishaji.

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras na waziri wa fedha Euclid Tsakalotos
Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras na waziri wa fedha Euclid TsakalotosPicha: picture-alliance/dpa/P. Saitas

Hata hivyo bado yapo masuala yanayohitaji ufumbuzi, ikiwa pamoja na msamaha wa kodi kwa visiwa vya Ugiriki, bajeti ya ulinzi ya nchi hiyo, pamoja na matakwa ya kufutiwa kiasi cha Euro Bilioni 320 katika deni lake.

Kupunguziwa deni

Waziri wa fedha wa Ugiriki, Euclid Tsakalotos amesema anaamini maombi ya nchi yake juu ya kupunguziwa deni yatakubaliwa na viongozi wa Ukanda wa Euro.Waziri Tsakalotos amesema anao uhakika kwamba Ugiriki itaruhusiwa kulihamishia deni lake la Euro Bilioni 27 kwa kwenye mfuko wa uokozi. Deni hilo linatokana na dhamana zake zinazoshikiliwa na Benki Kuu ya Ulaya, ECB

Waziri Mkuu wa Ugiriki Tsipras amesema mpango mpya uliopendekezwa na serikali yake ni mzuri zaidi kwa watu wa Ugiriki. Amesema mpango wa safari hii unatafautiana na ule wa wakopeshaji ambao haukujumuisha kupunguziwa deni.

Mwandishi : Mtullya Abdu/afp,dpa,

Mhariri: Caro Robi