1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki kuwasilisha mapendekezo mapya juu ya kuyalipa madeni yake

Abdu Said Mtullya11 Februari 2015

Ugiriki leo itayawasilisha mapendekezo madhubuti kwa wadai wake juu ya kuyalipa madeni yake ili nchi hiyo ipatiwe fedha kwa ajili ya kuyakidhi mahitaji yake.

https://p.dw.com/p/1EZRV
Waaziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis TsiprasPicha: picture alliance

Pamoja na mapendekezo itakayoyawaslisha mjini Brussels leo,Ugiriki inaitaka Benki Kuu ya Ulaya ECB, itoe Euro Bilioni 1.9 ambazo ni faida iliyotokana na kuuzwa dhamana za Ugiriki. Ugiriki pia inaitaka Benki kuu hiyo itoe mkopo wa muda mfupi wa kiasi cha Euro Bilioni 8 kwa Ugiriki ili iweze kuyakidhi mahitaji yake ya haraka.

Nchi hiyo yenye madeni makubwa pia inataka iruhusiwe kunufaika na mfuko wa fedha ulioanzishwa maalum na Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kuisaidia Ugiriki.

Ugiriki inayaita mapendekezo hayo kuwa ni hatua za muda zitakazoiwezesha nchi hiyo kuendelea na shughuli zake mpaka hapo itakapofikia makubaliano na wadai wake juu ya mpango mpya wa kuyalipa madeni yake.

Mpango wa maafa

Msemaji wa serikali ya Ugiriki ameeleza kuwa hatua hizo za muda mfupi zitaipa nchi yake muda wa kuutayarisha mpango wa miaka minne wa kuyalipa madeni yake. Waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis ameuita mpango wa Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF(Troika) kuwa ni wa maafa na nchi yake inakusudia kuikataa thuluthi nzima ya mpango huo.

Juu ya mkutano wa leo Rais wa Halmshauri ya Umoja wa Ulaya Jean- Claude Juncker amesema ni juu ya Ugiriki kuwasilisha mapendekezo yenye maudhui yatakayoleta mapatano. Lakini kiongozi wa wabunge wa vyama vya mrengo wa kushoto kwenye Bunge la Ulaya Gabi Zimmer amesema demokrasia imo hatarini barani Ulaya kutokana na ung'ang'anizi wa sera ya kubana matumizi.


Mbunge huyo amesema viongozi wa Umoja wa Ulaya bado hawajatambua, kwamba tokea siku nyingi "tunakabiliwa" ,siyo tu na mgogoro wa madeni na wa kiuchumi bali migogoro hiyo inatangamana na mgogoro wa demokrasia katika Umoja wa Ulaya."

Wagiriki zaidi ya Milioni 2.5 ni masikini sana

Afisa mmoja kwenye wizara ya fedha ya Ugiriki amearifu kwamba nchi yake inawasiliana na shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo OECD ili kupendekeza mpango mwingine wa mageuzi utakaopunguza umasikini na ukosefu wa ajira nchini Ugiriki.

Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras aliwaambia wabunge wa nchi yake mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba Wagiriki Milioni 1.5 hawana ajira na zaidi ya milioni 2.5 wanaishi katika umasikini mkubwa .

Mawaziri wa fedha wa ukanda wa sarafu ya Euro wanakutana muda mfupi tu baada ya Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras kushinda kura ya imani juu ya kuubatilisha mpango wa Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya,ECB na Shirika la fedha la kimataifa juu ya kuikoa Ugiriki.

Mwandishi:Mtullya Abdu.ZA,apf.

Mhariri:Gakuba Daniel