1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza imeanza kutoa chanjo ya Covid-19

8 Desemba 2020

Maafisa wa afya nchini Uingereza leo Jumanne wameanza kutoa dozi za kwanza za chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 na kuanza rasmi mpango wa kimataifa wa chanjo ambao unatarajiwa kushika kasi katika siku za hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/3mOCY
Großbritannien Coronavirus Covid-19 Impfung
Margaret Keenan, amekuwa mtu wa kwanza kupokea chanjo ya Covid-19Picha: Jacob King/PA Wire/empics/picture alliance

Hatimaye ulimwengu una matumaini ya kuutokomeza kabisa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya Corona. Hii ni baada ya Uingereza kuanza rasmi zoezi la kutoa chanjo kwa raia wake leo Jumanne.

Margaret Keenan, ambaye wiki ijayo atatimiza miaka 91 amekuwa wa kwanza kupokea chanjo hiyo katika hospitali ya chuo kikuu cha Coventry, hospitali hiyo ikiwa moja ya vituo vya afya ambavyo vimeanza programu ya kutoa chanjo hiyo.

Keenan amesema chanjo hiyo ni kama zawadi ya mapema ya maadhimisho yake ya siku ya kuzaliwa.

Maafisa wa afya wamesema dozi za kwanza 800,000 zitapeanwa kwa watu walioko katika hatari ya kuambukizwa virusi vya Corona kama vile wazee wenye zaidi ya umri wa miaka 80, pamoja na wauguzi wa nyumbani.

Maafisa hao wa afya wametoa wito kwa umma kuwa wavumilivu hadi angalau mwaka ujao. Waziri wa afya wa Uingereza Matt Hancock amesema: "Kuanzia Jumanne, ambayo imepewa jina la V Day, tutaanza kutoa chanjo ya Covid 19 kote Uingereza. Na huu ndio mwanzo wa mwisho wa janga hili. Bado hatujafika, lakini ni muhimu ili watu waendelee kufuata maelekezo tutakayowaagiza, kama vile kufuata sheria ili kuhakikisha tunadhibiti kasi ya maambukizi ili mwishowe tupate mafanikio."

Ujerumani kujadili upya vikwazo zaidi vinavyonuia kuzuia kusambaa kwa Covid-19

Kanzlerin Merkel, Ministerpräsidentensitzung
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Markus Schreiber/AP/picture-alliance

Na nchini Ujerumani, Waziri wa afya Jens Spahn amesema Ujerumani huenda ikalazimika kuweka vikwazo zaidi ili kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa wa Covid-19.

Kauli ya waziri huyo wa afya anaitoa katika wakati ambapo maambukizi yanaendelea kuongezeka kila kukicha licha ya serikali kusitisha kwa muda baadhi ya shughuli za kiuchumi kuanzia mwanzoni mwa mwezi Novemba.

Serikali kuu na viongozi wa majimbo 16 ya Ujerumani wanatarajiwa kufanya tena mkutano ili kujadili hatua kali zaidi zinazonuia kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Mkuu wa jimbo la Bavaria Markus Soeder amesema: "Kwa sasa hali ni mbaya sana. Hivi vikwazo havitoshi, lazima tufanye zaidi, lazima tuchukue hatua. Na ndio maana nimeitisha mkutano maalum kujadili vikwazo vipya kabla ya sikukuu ya krismasi ili kupambana na kuenea kwa virusi vya Corona"

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema kuwa vikwazo vilivyowekwa sasa havitatosha kupunguza idadi ya maambukizi, kwa hiyo hatua zaidi zinafaa kuchukuliwa.