1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza: Kinyang'anyiro cha kumrithi Theresa May chaanza

Zainab Aziz
10 Juni 2019

Kinyang'anyiro cha uongozi wa Chama cha Kihafidhina kimeanza rasmi leo Jumatatu baada yaTheresa May kung'atuka uongozini mnamo siku ya Ijumaa. Mshindi atachukua nafasi ya bibi May kama Waziri Mkuu wa Uingereza.

https://p.dw.com/p/3K7qr
Brexit
Picha: picture-alliance/empics

Waziri wa zamani wa mambo ya nje Boris Johnson ndiye mwenye nafasi nzuri ya kushinda lakini Waziri wa Mazingira Michael Gove ni mgombea mwenye nguvu pia. Wagombea 11 wa chama cha Kihafidhina nchini Uingereza wanawania kumrithi Waziri Mkuu Theresa May katika uongozi wa chama hicho kikongwe. Mchakato wa Brexit ndio hasa uliosababisha kuondoka uongozini bibi Theresa May na unatarajiwa kuwa mjadala mkubwa kati ya wagombea hao wanaowania kumrithi. Kiongozi wa zamani wa chama hicho Theresa May bado ni Waziri Mkuu.

Wajumbe wa chama cha Kihafidhina wa bunge la Uingereza leo wataipokea orodha ya wenzao wanaotaka madaraka ya juu katika chama chao baada ya uwasilishaji wa nyaraka za kugombea utakapokuwa umekamilika na hatimaye kamati ya mwaka 1922 ya wabunge wa chama cha Kihafidhina itaweka weka wazi orodha ya wagombea ambao wamefanikiwa kuingia katika kinyang'anyiro hicho.

Miongoni mwa wagombea wanaotaka kumrithi Theresa May

*Waziri wa zamani wa mambo ya nje na aliyekuwa Meya wa jiji la London Boris Johnson

*Waziri wa mambo ya Nje Jeremy Hunt

*Waziri wa mambo ya ndani Sajid Javid

* Kiongozi wa zamani wa Bunge Andrea Leadsom

Kushoto: Michael Gove.Kulia: Boris Johnson
Kushoto: Michael Gove.Kulia: Boris JohnsonPicha: picture-alliance/S. Rousseau

Kutokana na idadi kubwa ya wanaotaka kugombea, kutakuwepo duru kadhaa za upigaji kura kati ya wabunge 313 wa chama hicho ili kupunguza idadi hiyo. Wagombea wawili watakaobaki watapigiwa  kura na wanachama wa chama hicho cha Kihafidhina, wapatao 150,000.

Ili kuwavutia wajumbe wa chama cha Kihafidhina wenye msimamo mkali, wagombea wote wanadai kwamba wanaweza kufanikisha kuiondoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya kwa njia bora kuliko mpango wa bibi Theresa May. Wengi wao wamesema wataiondoa Uingereza kutoka kwenye umoja huo kufikia mwisho wa mwezi Oktoba hata ikiwa bila ya mkataba.

Boris Johnson amesema iwapo atachaguliwa atakataa kulipa madeni yaliyokubaliwa na Uingereza kwa Umoja wa Ulaya katika kipindi cha uanachama wake.

Uamuzi juu ya nani hasa atakayekiongoza cha Kihafidhina unatarajiwa mwishoni mwa mwezi Julai, muda mfupi tu ambapo kiongozi mpya atalihutubia Bunge na baada ya hapo Bunge hilo litakwenda likizo ya majira ya kiangazi hapo mwezi Agosti na litarejea tena mwanzoni mwa Septemba.

Chanzo://p.dw.com/p/3K7PR

Mhariri: Mohammed Khelef