1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa Ujasusi wa Rwanda aachiwa huru na Uingereza

11 Agosti 2015

Mahakama ya Uingereza imemuachia huru mkuu wa shirika la ujasusi wa Rwanda Jenerali Emmanuel Karenzi Karake anayetakikana na Uhispania kwa madai ya kuhusika katika uhalifu wa kivita wakati wa mauaji ya halaiki Rwanda.

https://p.dw.com/p/1GDNM
Picha: J. Tallis/AFP/Getty Images

Mahakama hiyo imesema imemuachia huru Jenerali Karenzi Karake kwasababu haina mamlaka ya kumhukumu baada ya kushauriwa kuwa sheria iliyotumiwa kumkamata Karenzi na kumtaka kusafirishwa Uhispania kujibu mashitaka ya ugaidi haiwahusu watu wasio wakaazi wa Uingereza.

Idara ya kusimamia shughuli za uendesha mashitaka Uingereza CPS iliyokuwa ikishughulikia kesi hiyo kwa niaba ya idara ya mahakama ya Uhispania kuambatana na kesi kuhusu kusafirishwa kwa mtuhumiwa kujibu mashitaka imesema Jaji Howard Riddle ameiondoa kesi hiyo baada ya kupokea ushauri kutoka kwa CPS.

Uhispania yamtaka Karake

Askari wa Uingereza walimkamata Jenerali huyo mwenye umri wa miaka 54 mnamo tarehe 22 mwezi Juni katika uwanja wa ndege wa Heathrow kufuatia kibali cha kutaka kukamatwa kwake kilichotolewa na Uhispania.

Wanajeshi wa Rwanda wakielekea katika operesheni ya kulinda amani CAR
Wanajeshi wa Rwanda wakielekea katika operesheni ya kulinda amani CARPicha: Getty Images/AFP/E. Musoni

Karake alikuwa kamanda wa kijeshi katika kundi la waasi la Rwandan Patriotic Front RPF ambalo lilifanya operesheni kubwa mwaka 1994 kukomesha mauaji ya halaiki yaliyosababisha vifo vya watu laki nane wengi wao wa kutoka kabila la watutsi. Hivi sasa RPF ndiyo chama tawala nchini Rwanda.

Jaji wa mahakama ya Uhispania mnamo mwaka 2008 alitoa kibali cha kukamatwa kwa viongozi 40 wa kijeshi wa Rwanda akiwemo Karake ambaye anadaiwa aliamuru kuuawa kwa raia watatu wa Uhispania mwaka 1997 waliokuwa wakifanya kazi na shirika moja la kutoa misaada ya kiafya.

RPF imekanusha kuwa Karake na makamanda wenzake wa jeshi walihusika katika uhalifu wa kivita baada ya mauaji hayo ya halaiki. Kukamatwa kwake nchini Uingereza kuliighadhabisha mno serikali ya Rwanda ambayo ilikitaja kitendo hicho udhalilishaji na hujuma zinazolenga kuiabisha Rwanda. Umoja wa Afrika pia ulikuwa umetaka mkuu huyo wa shirika la ujasusi wa Rwanda kuachiwa huru mara moja bila ya masharti yoyote.

Rwanda yafurahishwa na kuachiwa huru kwa Karake

Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Louise Mushikwabo kupitia ukurasa wake wa Twiiter amesema amefurahishwa na kuachiwa huru kwa Karake na kuwa anarejea nyumbani. Mushikwabo amekiita kisa cha kukamatwa kwake mchakato dhalimu ambao haukupaswa kuwepo.

Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo
Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Louise MushikiwaboPicha: picture-alliance/dpa

Mahakama ilikuwa imempa dhamana Karake mnamo tarehe 25 mwezi Juni akisubiri kutekelezwa kwa mchakato wa kusafirishwa hadi Uhispania kujibu mashitaka ya ugaidi. Miongoni mwa mawakili waliomuwakilisha ni Cherie Blair ambaye ni mke wa aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair.

Ripoti za kukinzana zimeibuka kuhusu hasa ni kipi kilichojiri Rwanda na eneo la mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ambako wapiganaji wa kihutu wanaotuhumiwa kufanya mauaji ya halaiki walikimbilia mwaka 1994 na kuandamwa na vikosi vya majeshi ya Rwanda.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters

Mhariri:Iddi Ssessanga