1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yatuma maombi EU kuchelewesha Brexit

Zainab Aziz Mhariri: Angela Mdungu
21 Oktoba 2019

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ametuma barua tatu kwa Umoja wa Ulaya. Johnson alituma barua hizo Jumamosi jioni mara baada ya Bunge la Uingereza kupiga kura ya kuchelewesha kuufanyia uamuzi mpango wake wa Brexit.

https://p.dw.com/p/3RaBQ
Großbritannien Brexit Boris Johnson
Picha: imago images/PA Images/M. Crossick

Barua ya kwanza kutoka kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson imetumwa kwa Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk. Barua hiyo ambayo haikutiwa saini na Waziri Mkuu Johnson ni nakala ya rasimu iliyomo katika sheria za Uingereza inayomlazimu Waziri Mkuu kuomba kurefushwa muda wa mchakato wa Brexit.

Barua ya pili iliyopelekwa kwa Umoja wa Ulaya ni kuhusu pingamizi la Waziri Mkuu huyo wa Uingereza dhidi ya kurefushwa muda wa Brexit. Bwana Johnson amesema kurefushwa muda wa mazungumzo ya mchakato wa Brexit litakuwa ni kosa kubwa.

Na ya tatu imetoka kwa Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya Tim Barrow na kupelekwa kwa Jumuiya hiyo ya Umoja wa Ulaya kwa niaba ya Waziri Mkuu Boris Johnson. Ujumbe wa Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson uliomo kwenye barua hiyo iliyochapishwa kwenyeTwitter na mwandishi mmoja wa gazeti la Financial Times mjini Brussels unasema.

"Nimeweka wazi tangu nilipochukuwa madaraka ya Uwaziri Mkuu na nimerudia hayo kwa wabunge siku ya Jumamosi kwamba maoni yangu, na msimamo wa serikali yangu, kuhusu kuongeza zaidi wa mchakato wa Brexit kutaharibu masilahi ya Uingereza na ya washirika wetu wa Umoja wa Ulaya, na kwamba hatua hiyo itavuruga uhusiano kati yetu."

Maandamano yaliyofanyika jijini London ya kutaka kura nyingine ya maoni kuhusu Brexit
Maandamano yaliyofanyika jijini London ya kutaka kura nyingine ya maoni kuhusu BrexitPicha: Getty Images/AFP/N. Halle'n

Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk amethibitisha kupokea barua ya maombi ya kurefushwa mchakato wa Brexit na amesema ataanza kujadili suala hilo na viongozi wa Umoja wa Ulaya.

Wakati huo huo, maelfu ya watu waliandamana mjini London siku ya Jumamosi wakitaka kura nyingine ya maoni kuhusu nchi hiyo kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya. Waandamanaji hao walisherehekea pia hatua ya bunge la nchi hiyo kupiga kura ya kuahirisha kwa muda mchakato wa Brexit. Wengi wa waandamanaji hao walisafiri umbali mrefu kutoka maeneo mbalimbali ya Uingereza hadi jijini London kushiriki kwenye maandamano hayo. 

Chanzo: https://p.dw.com/p/3Ra5A