1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Armin Laschet ni mwenyekiti mpya wa CDU

Daniel Gakuba
16 Januari 2021

Waziri Mkuu wa jimbo la Nord Rhine-Westphalia Armin Laschet amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, na kujiweka katika nafasi ya kurithi ukansela wa Ujerumani baada ya Angele Merkel.

https://p.dw.com/p/3o0rn
CDU Digitaler Parteitag Laschet wird Vorsitzender
Armin Laschet, mwenyekiti mpya wa chama cha CDUPicha: Hannibal Hanschke/REUTERS

Laschet amewaangusha washindani wawili, mfanyabiashara mwenye mrengo mkali wa kihafidhina Friedrich Merz, na mkuu wa masuala ya nje katika chama cha CDU, Norbert Roettgen.

Katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo uliofanyika Jumamosi kwa njia ya mtandao, Merz aliongoza akipata kura 385, akimpita kwa kura tano tu Laschet aliyepata kura 380. Roettgen alienguliwa kwa kuambulia kura 224.

Soma Zaidi: Chama cha CDU chakutana kuelekea uchaguzi wa kiongozi wao

Hata hivyo Laschet anayeliongoza jimbo lenye idadi kubwa zaidi ya watu nchini Ujerumani aliibuka mshindi katika duru ya pili, akipata kura 521 dhidi ya 466 zilizomuendea Merz.

Deutschland CDU-Vorsitz Kandidaten Laschet Röttgen Merz
Armin Laschet (katikati) na wapinzani aliowashinda; Friedrich Merz (kushoto) na Norbert Roettgen (kulia).Picha: Andreas Gora/Getty Images

Armin Laschet mwenye umri wa miaka 59 na mshirika mwaminifu kwa kansela Angela Merkel, anayo nafasi kubwa ya kumrithi Merkel anayeondoka katika wadhifa huo mwezi Septemba, baada ya kuushikilia kwa mihula minne.

Macho sasa yanaelekezwa katika uchaguzi wa shirikisho

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Laschet amesema atafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa chama chake kinapata matokeo mazuri katika uchaguzi mkuu ujao, ili kiendelee kushikilia wadhifa wa ukansela.

Amewasifu pia wapinzani wake katika uchaguzi wa leo kwa kushindana kwa njia sahihi.

Soma zaidi: Merkel asema hatoshawishi chaguo la mrithi wake

Friedrich Merz aliyekuja katika nafasi ya pili amempongeza Laschet akimtakia majukumu mema kama mwenyekiti mpya wa CDU, na kuungana naye kutaka juhudi kubwa za kichama kuelekea uchaguzi unaofuata.

Laschet Pia amepongezwa na kiongozi wa chama ndugu cha Christian Social Union (CSU) cha jimboni Bavaria, Markus Soeder, ambaye amesema anatarajia wataendeleza ushirikiano wenye mafanikio.

Merkel anatarajiwa kustaafu siasa mwishoni mwa muhula wake huu, na hadi uchaguzi utakapofanyika atakuwa ameiongoza serikali ya Ujerumani kwa miaka 16. 
 

dpae, ape