1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na China zaimarisha mahusiano

30 Oktoba 2015

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri mkuu wa China Li Kenqiang wameongoza utiaji saini mikataba 15 ya kibishara wakati wa ziara katika mkoa wa mashariki wa Anhui siku ya Ijumaa.

https://p.dw.com/p/1GxGq
Kansela Merkel na waziri mkuu wa China Li Kenqiang.
Kansela Merkel na waziri mkuu wa China Li Kenqiang.Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Eisele

Makampuni ya Kichina yalisaini mkataba wa ununuzi wa helikopta 100 kutoka kampuni ya ndege ya Ulaya Airbus kwa kiasi cha karibu euro bilion moja, ambazo ni sawa na dola bilioni 1.1. Kiwanda cha utengenezaji wa helikopta hizo aina ya H135 kitaanzishwa nchini China kama sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa.

Hii ndiyo mara ya kwanza kwa waziri mkuu Li kumualika kiongozi wa nje kutembelea mkoa wake wa uzawa, jambo ambalo linachukuliwa kuwa heshima kwa mgeni husika. Awali Merkel alishiriki sherehe za ya miaka 30 ya ubadilishanaji kati ya chuo cha mkoa huo cha Hefei na vyuo vikuu vya Ujerumani.

Alitarajiwa kukitembelea kijiji cha Shen Fu baadae siku ya Ijumaa kujifunza kuhusu juhudi za vijiji vya China kupunguza umaskini, kabla ya kushiriki katika mkutano wa wafanyabiashara wa China na Ujerumani.

Siku ya Alhamisi Kansela Merkel na waziri mkuu Li waliongoza hafla kadhaa za utiaji saini makubaliano, yakiwemo ya ununuzi wa ndege na makampuni ya China kutoka Airbus yenye thamani ya dola bilioni 17. Pia siku ya Alhamis Merkel alielezea wasiwasi kuhusu mvutano wa maeneo kati ya China na majirani katika bahari ya China Kusini.

Kansela Merkel akizungumza na watoto wa shuke ya Jinputao katika kijiji cha Xinnacun, wilayani Baohe katika mkoa wa Hefei, China siku ya Ijumaa.
Kansela Merkel akizungumza na watoto wa shuke ya Jinputao katika kijiji cha Xinnacun, wilayani Baohe katika mkoa wa Hefei, China siku ya Ijumaa.Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Eisele

"Huwa nashangazwa kwa nini katika suala hazitumiki mahakama za kimataifa kutafuta suluhisho," alisema Merkel. Wasiwasi uliongezeka wiki hii baada ya Marekani kutuma meli ya kivita katika eneo la umbali wa kilomita 12 za baharini nje ya visiwa vya Spratly, ambavyo beijing inadai ni vyake kwa jina la Nasha.

"Tunaomba njia za biashara ya baharini ziendelee kuwa salama na huru, kwa sababu ni muhimu kwa kila moja katika eneo hilo," alisema Merkel.

Kansela Merkel alisema kimsingi Ujerumani iko tayari kuzingatia kuipatia China hadhi ya uchumi wa masoko kwa sharti la kufanyiwa tathmini na Umoja wa Ulaya.

Ujerumani ndiyo mshirika mkuu wa kibiashara wa China barani Ulaya, ambapo chama cha wafanyabiashara wa Ujerumani kiliripoti kuwa biashara kati ya mataifa hayo mawili ilifikia rekodi ya juu kabisaa mwaka 2014.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,rtre

Mhariri: Saumu Yusuf