1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani hairidhishwi na utekelezaji wa makubalino ya Minsk

Caro Robi4 Machi 2016

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amezishutumu Urusi na Ukraine kwa kukosa kutekeleza kikamilifu makubaliano ya kusitisha mapigano na kutafuta amani mashariki ya Ukraine.

https://p.dw.com/p/1I74y
Picha: Reuters/J.Naegelen

Katika mazungumzo ya faragha kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Ufaransa, Urusi na Ukraine mjini Paris hapo jana, Steinmeier amesema hajaridhishwa na jinsi Urusi na Ukraine zinavyoyashughulikia makubaliano ya Minsk.

Steinmeier amesema anahofia kuwa hali ya mashariki ya Ukraine haichukuliwi kwa uzingativu upasao na ghasia huenda zikaongezeka tena wakati wowote. Mawaziri hao wa mambo ya nje walikutana kwa saa tisa ili kujaribu kufikia maufaka wa kupatikana amani mashariki mwa Ukraine huku serikali ya Ukraine ikikabiliwa na mivutano ya kisiasa.

Mageuzi kamili bado mashariki ya Ukraine

Ujerumani imesema licha ya kuwa ghasia zimepungua mashariki ya Ukraine, bado mageuzi ya kijamii na kiuchumi hayajashughulikiwa. Steinmeier na mwenzake wa Ufaransa Jean Marc Ayrault wamekuwa wakizishinikiza Ukraine na Urusi kupiga hatua katika kufikia suluhisho la kudumu kuhusu mzozo wa Ukraine.

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier
Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter SteinmeierPicha: DW/M.Hofmann

Mazungunzo hayo yalidhamiria pia kuangazia uwezo wa Ukraine wa kutimiza matakwa ya kisiasa kuambatana na makubaliano ya Minsk ambayo yalifikiwa mwezi Februari mwaka jana. Mawaziri hao wamekubaliana kuwa chaguzi muhimu pia zifanywe mashariki ya Ukraine ifikapo mwishoni mwa mwezi Julai.

Ayrault amesema mkutano huo wa Paris umepiga hatua katika kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Ukraine na wanasisitiza umuhimu wa kuidhinisha sheria za uchaguzi ili kuweza kuandaliwa chaguzi. Hata hivyo Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Pavlo Klimkin amesisitiza kuwa hakutafanyika chaguzi mashariki mwa nchi hiyo hadi kukomeshwe kikamilifu uhasama kati ya serikali na waasi wanaotaka kujitenga kwa eneo hilo.

Huku nchi za magharibi zikiwa na mtizamo kuwa kufanyika chaguzi itakuwa ni fursa kwa eneo hilo kurejea katika siasa za kitaifa, Ukraine ina wasiwasi kuwa Urusi ambayo inashutumiwa kwa kuwaunga mkono waasi itatumia chaguzi hizo kuiyumbisha zaidi Ukraine.

Urusi yatiliwa shaka

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov aliondoka katika mkutano huo bila ya kuzungumza na waandishi wa habari. Wanadiplomasia hao pia wametaka kuachiwa na kubadilishana kwa wafungwa na watu wote wanaozuiwa kinyume cha sheria kati ya sasa hadi tarehe 30 mwezi Aprili.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa zaidi ya watu 9,000 wameuawa katika mzozo huo wa Ukraine ulioanza mwaka 2014. Awali hapo jana, ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu ilisema watu milioni tatu wanakumbwa na hali ngumu na kutengwa kisiasa,kijamii na kiuchumi mashariki ya Ukraine kutokana na mzozo.

Umoja wa Mataifa umeongeza watu katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi mashariki mwa Ukraine wanakabiliwa na mateso na kuzuiwa kiholela.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/afp

Mhariri: Iddi Ssessanga