1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuheshimu ahadi yake kwa NATO

Friedel Taube5 Juni 2013

Ujerumani imesema itasimamia ahadi yake ya kusaidia ufadhili wa ndege zisizotumia rubani za Jumuiya ya kujihami ya NATO, licha ya nchi hiyo kufuta mpango wake wa kununua ndege zake yenyewe.

https://p.dw.com/p/18jol
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Thoma De Maziere mbele ya mfano wa ndege ya Euro hawk isiyotumia rubani.
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Thoma De Maziere mbele ya mfano wa ndege ya Euro hawk isiyotumia rubani.Picha: Reuters

NATO inapanga kuanzishwa mfumo wa uchunguzi  unaojulikana kama AGS kwa kutumia ndege tano aina ya "Global Hawk 40" na waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maiziere, alisema wakati wa mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa NATO mjni Brussels, kuwa nchi yake itaheshimu makubaliano iliyoyasaini.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere.Picha: Getty Images

Tarehe 14 Mei Ujerumani ilifuta mpango wake wa kununua ndege za uchunguzi zisizo na rubani chapa ya Euro Hawk, zinazotenegenezwa na kampuni ya EADS ya Ulaya na Northrop Grumman ya Marekani kutokana na gharama. Waziri De Maiziere leo atahojiwa na kamati ya Bunge mjini Berlin kuhusiana na mpango huo uliyofutwa. Wanasiasa wa upinzani wanasema kiasi cha euro 680 milioni zimetumiwa katika mradi huo uliofeli.

Kuchangia euro milioni 483 kwa mradi wa NATO

Uamuzi wa kujiondoa katika ununuzi wa ndege ulizua masuali iwapo Ujerumani ingeendelea kuunga mkono mpango wa NATO kununua ndege zake za uchunguzi, pia kutoka kampuni ya Northrop Grumman, kama sehemu ya mradi wa uchunguzi wa pamoja (AGS). Kamati ya bajeti ya bunge la Ujerumani iliidhinisha euro milioni 483 mwaka uliyopita, kama mchango wa nchi hiyo kwa mradi wa ndege zisizo na rubani za NATO.

Vyama vya upinzani vinamtuhumu de Maiziere, mshirika wa karibu wa Kansela Angela Merkel kwa kuhodhi taarifa kuhusiana na kufutwa kwa mpango wa ununuzi wa ndege hizo, miezi minne kabla ya kufanyika kwa uchaguzi. Mpinzani mkuu wa Merkel katika uchaguzi wa Septemba 22 Peer Steinbrück amesema jana mjini Berlin kuwa Ujerumani haihitaji ndege hizo. Jeshi la Ujerumani tayari linayo ndege moja aina ya Euro Hawk na lilikuwa linatafakkari kununua nyingine nne. Serikali ilikuwa imetenga euro bilioni 1.2 kwa ajili ya kununua na kuendeleza ndege hizo, lakini jeshi lilisema halitanunua tena ndege hizo kwa sababu hazikidhi mahitaji ya usalama.

Ndege ya awali iliyouzwa kwa Ujerumani ikiwa imeegeshwa katika uwanja wa kijeshi wa Jagel nchini Ujerumani.
Ndege ya awali iliyouzwa kwa Ujerumani ikiwa imeegeshwa katika uwanja wa kijeshi wa Jagel nchini Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa

Kampuni ya Northrop Grumman ilisaini mkataba na NATO wenye thamani ya karibu euro bilioni moja mwezi Mei mwaka 2012, kwa ajili ya mfumo mpya wa uchunguzi, ambao utajumuisha ndege tano zisizo na rubani na vituo vya ardhini vinavyohamishika. Wanachama 14 wanaounda Jumuiya ya NATO ikiwemo Ujerumani, walikubali kulipia mfumo huo mpya, ambao utakuwa tayari kati ya mwaka 2015 na 2017,  na ambao NATO itauendesha na kuusimamia kwa niaba ya washirika wote 28 wa jumuiya hiyo.

Kwanini hakuna mradi wa Ulaya?

Ndege za Global Hawk zinaweza kuruka juu kiasi cha kilomita 20 na katika umbali huo bado zinakuwa na uwezo wa kuchukua picha zinazoonekana vizuri sana, na kuwezesha ufuatiliaji wa wahusika. Mradi wa NATO utaendelea licha ya Ujerumani kusimamisha wa kwake, lakini hali nchini Ujerumani imekosolewa mjini Brussels.

Michael Gahler, msemaji wa usalama wa chama cha kihafidhina cha EPP katika bunge la Ulaya, anasema Ujerumani ilipaswa kutafuta suluhisho kupitia Umoja wa Ulaya kuliko kufanya kivyake, kwa kuzingatia kuwa mataifa ya Ulaya yanakabiliwa na changamoto sawa za kiusalama na kila taifa halina fedha za kutosha kufanya kivyake. "Miradi kama hiyo ni mifano mizuri ya namna mambo kama hayo yanaweza kufanyika kwa ushirikiano - hasa wakati kitu kipya kinapokuwa kinatengenezwa. Nadhani kila mmoja atajifunza kutokana na kosa hilo."

Kampuni ya Northrop imejitetea dhidi ya malalamiko ya Ujerumani, baada ya Berlin kulalamika juu ya ukosefu wa kifaa kinachoweza kuzuia ndege hizo kugongana na kukosekana na nyaraka muhimu kwa ajili ya kuidhinishwa kwa ndege hiyzo katika anga ya Ulaya. Msemaji wa kampuni hiyo aliliambia gazeti la kila wiki la 'Die Zeit', kwamba Ujerumani haikubainisha nyaraka za aina gani ilizozitaka, na kwamba ni ndege ya awali tu iliyofanya kazi bila kinga ya kugongana. Kampuni hiyo ilisema kifaa hicho kingewekwa katika ndege nne nyingine ambazo Ujerumani ilikuwa imeagiza.

Mwandishi: Hasselbach Christoph (HDG - Europa)
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Josephat Nyiro Charo